Taasisi za Serikali zimehimizwa ziwe karibu na wananchi ili ziweze kuwahudumia na kuwaelimisha juu ya huduma inazozitoa. Wananchi wengi wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kuhusu watumishi wa umma kutotumia weledi na ubunifu katika kuwahudumia wananchi jambo ambalo likiachwa liendelee, Tanzania itaachwa nyuma ndani ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na ulimwengu mzima kwa ujumla.

Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhan Mwinyi katika semina kuhusu elimu ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zake inayotolewa na wataalamu wa Wizara yake kisiwani Pemba. Semina hiyo iliyoanza jana inafanyika kwenye uwanja wa Gombani, Pemba na itamalizika tarehe 18 Mei 2017.

"Kuna fursa nyingi za kiuchumi katika Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini kama wananchi wetu hatutawasaidia na kuwaelimisha kuhusu nyaraka na masharti yanayokidhi vigezo wataachwa nyuma na kubaki kuwa watazamaji na walalamikaji" Balozi Mwinyi alisema.

Wajasiriamali walielezea masikitiko yao juu ya ugumu wa kupata hati za kusafiria kutokana na mlolongo wa masharti hususan, inapotokea kuwa safari ni ya ghafla. Aidha, wajasiriamali wamekuwa wakilalamika kuwa wanapata tabu kusajili bidhaa zao katika mamlaka zinazosimamia ubora wa viwango wa bidhaa, chakula na madawa kwa kuelezwa kwamba bidhaa zao ni duni, hivyo wameiomba Serikali iwawezeshe kupata teknolojia ya kisasa ikiwa ni pamoja na vifungashio.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi akitoa mwongozo kwa wajumbe wa semina ya Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki inayoendelea kufanyika kisiwani Pemba. Pamoja na mambo mengine amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa zinazopatikana kwenye mtangamano. 
Mbunge wa jimbo la Konga, Mhe. Mbarouk Ali akichangia jambo kwenye semina. 
Sehemu ya wajumbe wakiendelea kusikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikiendelea kutolewa kwenye semina. 
Afisa kutoka Ofisi za Uhamiaji Pemba Bw. Haji Kassim Haji akijibu hoja mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na wajumbe kwenye semina juu ya upatikanaji wa Hati ya Kusafiria ya Afrika Mashariki. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...