Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro amesema mwamko mdogo wa kielimu walionao Wananchi wengi ndio unaopelekea ongezeko kubwa la vitendo vya udhalilishaji vinavyoendelea kushuhudiwa kufanyika kila kukicha katika maeneo mbali mbali hapa nchini.
Alisema baadhi ya Watu wakorofi wamekuwa wakitumia udhaifu huo kwa kuendeleza vitendo viovu dhidi ya Wanawake na Watoto ambao huathirika kiakili na kimwili na kuwapa wakati mgumu wa kuendelea na maisha yao ya kawaida ndani ya Jamii inayowazunguuka.
IGP Simon Sirro alieleza hayo wakati alipofika Ofisini kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.
Kamanda Sirro alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba katika kukabiliana na vitendo hivyo viovu vinavyoonekana kuleta fadhaa inalazimika kwa Jamii wakati huu kubadilika kwa kuwa tayari kutoa ushahidi pale wanaposhuhudia vitendo hivyo.
Alisema kesi yoyote inategemea kuendeshwa katika misingi na taratibu za Kisheria kwa kuzingatiwa ushahidi unaotolewa na mashahidi ili haki inapotolewa iende sambamba na stahiki ya pande zote husika.
Kamanda sirro aliitahadharisha Jamii inayopenda kulalamika zaidi kwamba nje ya kukosekana kwa ushahidi wa tuhuma zozote zinazowasilishwa Polisi na hatimae kwenye Ofisi ya Muendesha Mashtaka maana yake hakuna kesi itakayoendelea hata kama kuna mtu aliyedhulumiwa.
Alisema zipo kesi nyingi za udhalilishaji hasa zile za utelekezaji wa familia zinazofanywa na baadhi ya Wanaume zaidi upande wa Tanzania Bara zinazofikia zaidi ya asilimia 80% na kusababisha familia husika kukosa matunzo jambo ambalo huchangia ongezeko la Watoto wa Mitaani wanaokosa malezi ya Familia.

“ Tunafarajika kuona kwamba ipo Sheria ya adhabu dhidi ya Watu wanaotupa na kutelekeza Familia zao kwa upande wa Tanzania Bara ambayo imekuwa ikitumika na kupunguza matukio kama hayo ”. Alisema Kamnada Simon Sirro.

Akizungumzia hali ya Amani Nchini Tanzania Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Nchi bado iko shwari licha ya matukio ya hapa na pale yanayoshuhudiwa katika Maeneo ya Rufiji.
IGP Sirro kupitia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi waendelee kushirikiana na vikosi vya ulinzi katika kutoa Taarifa za matukio ya uhalifu, Ujambazi na Uhujumu Uchumi kwenye maeneo yao ili vyombo vya Ulinzi vitumie maarifa yake katika kuwasaka wahalifu hao.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Ofisini kwake Vuga kujitambulisha Rasmi baada ya kuteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kushika wadhifa huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifafanua tatizo la Udhalilishaji dhidi ya Wanawake na Watoto linaloonekana kuathiri Jamii wakati akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Simon Sirro.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...