MKUU wa wilaya ya Ikungi mkoani Singida Miraji Mtaturu amewafuturisha waislamu wa wilaya hiyo huku akiwaasa kuendeleza tabia njema kwa mujibu wa kitabu cha Mwenyezi Mungu Quran hata baada ya mwezi Mtukufu wa Ramadhan kumalizika.

Akizungumza na waislamu hao baada ya kupata futuru wilayani humo Mtaturu alisema katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan watu wametenda mema yanayopaswa kuendeleza hata baada ya mwezi huo.

“Wakati tupo kwenye mfungo huu tupo kwenye darasa la tabia njema hivyo nawashauri hata baada ya mfungo huu tuyaendeleze,”alisema Mtaturu.Alisema serikali inafarijika pale inapoona wananchi wake wakifuata imani za dini zao na hivyo kuwa raia wema na nchi kuendelea kuwa na amani.

“Tunamaliza kukamilisha moja ya nguzo tano za uislamu panapo majaaliwa ya Mwenyezi Mungu,nawaombeni isiwe mwisho wa kufanya mema bali iwe ni mwendelezo katika siku zetu zote za maisha yetu,”alisisitiza Mtaturu.Mtaturu aliwatakia maandalizi mema ya sikukuu ya Eid El Fitri huku akiwaasa kusherehekea kwa amani,utulivu na upendo na kukumbuka kutoa Zaka kwa watu wasio na uwezo.

Alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kumuombea Rais Dokta John Magufuli kutokana na kazi kubwa anayoifanya katika kuendeleza dhamira yake ya kulinda rasilimali za nchi ili ziwanufaishe watanzania wote hasa wale wanyonge.

Kwa upande wake Sheikh wa wilaya hiyo Abdi Seleman akitoa neno la shukrani alimshukuru mkuu wa wilaya huyo kwa kuwafuturisha na kusema hiyo ni mara ya kwanza toka wilaya hiyo ianzishwe kwa mkuu wa wilaya kuwaalika futari.

“Kwa sadaka yako hii kwetu tunamuomba Mwenyezi Mungu akulipe kila la kheri,na inshallah huu usiwe mwisho bali uwe mwanzo wa kufanya hivi,”alisema Sheikh Seleman.

Nae Kadhi wa mkoa wa Singida Ramadhan Kaoja alimshukuru mkuu wa wilaya huyo na kusema hiyo ni dalili za kiongozi bora kwa kuwa karibu na jamii lakini pia ni sehemu ya kukamilisha imani yake ambapo kwa mwezi huu wa Ramadhan kwa kufuturisha anapata thawabu nyingi sana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...