Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii
Kwa mara nyingine tena mfanyabiashara Shabani Hussein maarufu kama "Ndama mtoto wa Ng'ombe" amekiri shtaka la utakatishaji wa fedha iliyofunguliwa na Jamhuri.
Ndama anayekabiliwa na mashtaka sita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, amekiri shtaka hilo la kutakatisha fedha ambazo ni dola za Marekani 540,000.


Kwa mujibu wa sheria ya kutakatisha fedha kifungu cha 12(a)na 13(1)(a) namba 12 cha 2016 mshitakiwa huyo anaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka isiyopungua mitano ama isiyozidi kumi au kulipa faini isiyopungua milioni 100 na isiyozidi milioni 500.
Ndama alishawahi kukiri kosa hilo lakini aliposomewa mashitaka yake maelezo ya awali, alikana shtaka na kesi yake kuamriwa iendelee kusikilizwa.
Wakili wa Serikali, Estazia Wilson amedai mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa kuwa kesi hiyo leo imekuja kwa ajili ya kutajwa hata hivyo, mshitakiwa Ndama aliomba mahakama kumkumbushia mashitaka yake ambapo kwa mara nyingine alikiri kosa la sita la utakatishaji fedha.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi ijumaa wiki hii (Julai 9, mwaka huu) kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Katika mashauri yaliyopita, upande wa utetezi katika kesi hiyo ukiongozwa na Wakili, Jeremiah Ntobesya waliomba upande wa mashitaka kurekebisha hati ya mashitaka ili kumsomea upya mteja wao kwa kuwa yaliyopo yana mapungufu.
Baadaye upande wa mashitaka ulifanya marekebisho ya hati ya mashitaka na kumsomea upya ambapo Ndama alikiri lakini kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali, alikana mashitaka.
Anadaiwa kuwa, kati ya Februari 26 na Machi 2014, Dar es Salaam, akiwa mwenyekiti na mtia saini pekee wa Kampuni ya Muru Platinum Tanzania Investment Limited na akaunti ya benki ya kampuni hiyo iliyoko kwenye Benki ya Stanbic alijihusisha moja kwa moja kwenye uhamishaji wa dola za Marekani 540,000 na kuzitoa huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la uhalifu la kujiapatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Licha ya kukubali mashitaka hayo, Ndama alikana makosa mengine yakiwemo ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. Mashtaka mengine yanayomkabili ndama ni, kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...