Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani ( wa pili kulia mbele) akimwongoza Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele (katikati mbele) kwenye ziara ya kukagua eneo la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji la Stiegler’s Gorge, Rufiji mkoani Pwani katika ziara hiyo.
Na Greyson Mwase, Rufiji.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani amesema Tanzania inatarajia kupata umeme wa uhakika wa Megawati 5000 ifikapo mwaka 2021, mara baada ya kukamilika kwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia  nguvu za maji katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji kwenye  eneo la Stiegler’s Gorge  lililopo  Rufiji mkoani Pwani ambao utaongeza umeme wa kiasi cha Megawati 2100 katika  gridi ya taifa.

Dk. Kalemani aliyasema hayo jana tarehe 29 Juni, 2017 katika ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka  Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo  ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji kutoka  Ethiopia kwenye eneo  la mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji ya Stieglers Gorge wilyani  Rufiji mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani akishuka kwenye boti kwa ajili ya kuelekea kwenye eneo la Stieglers Gorge kutakapojengwa mradi huo.

Wengine walioshiriki katika ziara hiyo ni pamoja na wataalam wa masuala ya  umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania,  Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini.  Ziara  hiyo inafuatia maombi ya  Rais John Magufuli kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia ya kutuma wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na  wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania.

Dk Kalemani alisema kuwa kupatikana kwa umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2021 kutachochea ongezeko la viwanda hivyo kuongezeka kwa fursa za ajira na biashara na kukuza uchumi wa nchi.
Alisema mradi huo mkubwa ni moja ya mikakati ya Serikali  kuhakikisha nishati inakuwa na mchango mkubwa katika  kufikia malengo  ya  Dira ya Maendeleo ya Taifa yenye lengo la kuhakikisha kuwa nchi inatoka katika orodha ya nchi maskini duniani na kuingia katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele (kushoto) akieleza jambo kwa Mhaidrolojia Mwandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Stanislaus Kizzy (kulia) katika ziara hiyo. Anayesikiliza katikati ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.

Alisisitiza kuwa mbali na mradi huo mkubwa, serikali imeweka mikakati ya kutumia vyanzo vingine vya nishati kama vile Gesi, Makaa ya Mawe, Jotoardhi, Upepo ili kuhakikisha kuwa nchi inapata umeme wa uhakika. Akielezea mafanikio ya mradi huo mbali na upatikanaji wa umeme wa uhakika, Dk. Kalemani alisema kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa shughuli za uvuvi katika mkoa wa Pwani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...