Na. Benjamin Sawe 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza mkaguzi kutoka ofisi yake kuchunguza hali ya upatikanaji wa dawa kwenye zahanati na kituo cha afya cha mjini Gairo mkoani Morogoro.

Akiwahutubia wananchi wa Gairo na vitongoji vyake Mh. Majaliwa alisema amechukua uamuzi huo baada Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dk. Albert Lyaruu kukiri kuwa baadhi ya watumishi wa Idara yake wanamiliki maduka ya dawa.

“Sasa ni lazima nilete mkaguzi kutoka ofisi yangu ili tupate picha halisi kama dawa zinazoletwa zinafika, na kama zinafika zinatumikaje.” alisema Waziri Mkuu.

Mh. Majaliwa alisema kumekuwa na baadhi ya watumishi wa afya wasiokuwa waaminifu kuchukua dawa katika vituo vya afya vya Serikali na kuzipeleka kwenye maduka yao hivyo kupelekea wananchi kukosa huduma za madawa katika hospitali za Serikali.

Alifafanua kuwa, Serikali haizuii watumishi wa afya kuwa na maduka ya dawa,bali inachokataa ni tabia ya baadhi ya watumishi wasiowaaminifu kuchukua dawa za Serikali na kuzipeleka kwenye maduka yao.

Katika Mkutano huo Dtk. Albert Lyaruu alisema amekuwa akipokea sh. milioni 109 kila robo mwaka na katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho amepokea kiasi cha fedha hizo na kati ya hizo asilimia 33 sawa na sh. milioni 36 zimetumika kununua dawa na vifaa tiba.

Aidha Mh. Majaliwa amewaagiza wahudumu wa afya kutokaa ofisini badala yake waende kwenye vituo vya afya na zahanati kuangalia na kusimamia matumizi ya dawa zinazotolewa na serikali akitolea mfano wa kesi ya mganga wa kituo cha afya cha Shinyanga kukutwa na dawa za Serikali nyumbani kwake.

Kuhusu sekta ya elimu Wilayani humo, Waziri Mkuu alisema Serikali imepeleka sh. milioni 419 ili kuongeza vyumba vya madarasa ikiwa ni pamoja na kupelekea sh. milioni 500 kwa kila Halmashauri kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu na sh. bilioni 1.2 ili kukamilisha ujenzi wa ofisi za halmashauri hiyo” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwahimiza wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kupata huduma za matibabu bila kulazimika kuwa na fedha taslimu pindi wanapougua wao wenyewe na familia zao.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa mji wa Gairo kwenye uwanja wa shule ya msingi Gairo ‘A’ uliofanyika Juni 3, 2017. Waziri Mkuu alikuwa wilayani humo kwa ziara ya siku moja. (Picha na OWM).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisikiliza maelezo yanayotolewa na Mbunge wa Gairo, Bw. Ahmed Shabiby kuhusu mradi wa maji wa mjini Gairo unaosimamiwa na MORUWASA ambao haujakamilika wakati alipofanya ziara ya siku moja wilayani humo, Juni 3, 2017. Kulia ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Eng. Gerson Lwenge. (Picha na OWM).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...