Na Mathew Kwembe

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare ameeleza kuwa mradi huo umepata mafanikio makubwa katika kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es salaam hususani katika barabara ya Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea kituo kikuu cha Kimara mwisho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma, Mhandisi Rwakatare alisema kuwa katika kipindi hicho cha mpito, Mabasi yaendayo haraka yameweza kusafirisha watu 200,000 kila siku kutoka watu 50,000 iliyokuwa ikisafirisha mwaka jana, wakati mradi unaanza.

Mhandisi Rwakatare alieleza kuwa Mradi huo umeweza kuokoa muda wa wananchi ambao kabla ya mradi kuanza walikuwa wakitumia usafiri mwingine uliokuwa ukichukua kutoka masaa mawili, wakati sasa wanatumia dakika 45 tu kwa safari ya kutoka Kimara hadi Posta kwa kutumia mabasi yaendayo haraka.

Alifafanua kuwa huduma hiyo mbali na kuwapunguzia mzigo wa nauli watumiaji wa kawaida wa mabasi ya daladala, mradi wa mabasi yaendayo haraka imeokoa gharama ya usafiri kwa wenye magari binafsi ambapo wengi wao wamekuwa wakiutumia zaidi usafiri huo.

Akizungumzia kuhusu maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma Mhandisi Rwakatare alisema kwa wakala umeona ni vyema kutumia maadhimisho hayo kusikiliza kero na maoni ya wananchi hasa watumiaji wa huduma hiyo ili kuona namna nzuri ya kuiboresha.

“Watumishi wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka wamekuwepo katika vituo vya Gerezani na Kimara mwisho kwa siku hizi mbili ili kusikiliza kero na maoni kutoka kwa wananchi wetu, na tunafurahi kuona huduma hii ikizidi kushika kasi, hasa kwa kuzingatia kuwa tupo katika kipindi cha mpito,” alisema.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare akiwasili katika Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka cha Kimara Mwisho. Mhandisi Rwakatare alipokewa na Kaimu Meneja Usafirishaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dkt Philemon Mzee (kushoto).
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare akipita sehemu ya ukaguzi wa tiketi na kadi zitumiwazo na Mabasi Yaendayo Haraka. Mhandisi Rwakatare alipata fursa ya kutembelea vitengo mbalimbali vya Kituo Kikuu cha Kimara mwisho na kujionea huduma za usafiri zinavyofanyika katika kituo hicho.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald Rwakatare akizungumza na mmoja wa abiria wa Mabasi yaendayo haraka katika Kituo Kikuu cha Mabasi hayo katika eneo la Kimara Mwisho.
Sehemu ya daraja linalotumiwa na wananchi pindi wanapoingia na kutoka katika Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka kilichopo Kimara Mwisho. Daraja hili ni miongoni mwa miundombinu iliyojengwa na Serikali kwa ushirikiano na Benki ya Dunia.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...