Na Dkt. Hamisi Kigwangalla.

 Kila siku nashuhudia wananchi wenzangu wakikalamika. Natamani kujibu. Naacha. Natamani kuwakumbusha wananchi wenzangu. Naacha. Nasema mbona sisi ni wepesi kusahau? Natamani kuwakumbusha wabunge wenzangu. Naacha. Nasema na mimi sasa nipo kwenye Serikali. Ni mtunga sera, ni mfanya maamuzi, nikisema watasema huyu ni 'Naibu Waziri'. Lakini kiukweli nina hamu na shauku ya kuzungumza na wananchi wenzangu. Nami nitoe yangu ya moyoni. Kama mwananchi mwingine yeyote yule tu. 

Nina haki hiyo. Na mimi haki yangu inalindwa na katiba na sheria za nchi yetu. Leo nimeona acha nipumue kidogo. Niseme. Niuvue userikali wangu. Niseme kama mwananchi mwingine yeyote yule. Nianze kwa kuweka wazi kabisa hapa, kwamba; haya ni yangu. Si ya Serikali. Serikali ni ya Rais Magufuli, tumempa dhamana, ndiyo. Hili halibishaniwi. Tumempa kazi, ndiyo. 

Hili pia halibishaniwi. Lakini kazi hii anaifanyaje? Tunazijua changamoto anazokumbana nazo? Je, ana nia ya kuzitatua? Ni maswali ambayo yanastahili majibu. Kwenye makala hii nitajaribu kuyafafanua kidogo kwa mtazamo wangu kadri nitakavyojaaliwa. Pamoja na kumpa dhamana Rais wetu, ni lazima tufahamu kuwa na sisi tuna wajibu wa kutimiza kwa Taifa letu. 

Tuna kazi ya kufanya kumsaidia Rais wetu kubeba mzigo wa kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kijamii kwenye Taifa letu. Tusimuachie huu mzigo peke yake. Tuubebe sote. Nchi ina changamoto nyingi sana, siyo kwamba Rais ama Serikali yake haizifahamu ama haina nia ya kuzitatua, ama Rais Magufuli amesinzia, ama anastarehe; kila siku anahangaika kukuna kichwa, usiku na mchana kuzitafutia ufumbuzi. Nadhani hili halina ubishani sana kwa mpenda kweli. 

Binafsi, sina shaka kabisa juu ya uwepo wa nia thabiti ya kuleta mapinduzi. Sina. Kwenye biashara ya kujenga nchi changamoto haziishi siku moja. Ukimaliza moja, nyingine inaibuka, na nyingine zinazaliwa kutokana na majawabu ya changamoto uliyoitatua. Juzi juzi hapa nilisema kuhusu mfumo wa afya wa nchi kubwa kama ya Marekani kuwa na changamoto ya kuwabagua watu maskini na wale wa tabaka la kati na kwamba unajenga matabaka makubwa sana yanayowanyima fursa sawa baadhi ya watu kwenye Jamii. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...