NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA .

OFISA Mtendaji wa Mtaa wa Mtakuja Kata ya Kishiri James Mwansyemela (39) amekamatwa kwa tuhuma za kushawishi na kupokea rushwa ya shilingi 200,000 kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa kifungu cha 15 (1a) akijifanya Mhandisi wa Jiji la Mwanza .

Mtuhumiwa huyo alikamatwa Juni 13 mwaka huu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza baada ya kuomba na kupokea rushwa hiyo kutoka kwa mfanyabiashara mmoja wa Mkolani jijini Mwanza ili asimwondoe kwenye eneo analofanyia biashara akidai ni hifadhi ya barabara.

Mkuu wa TAKUKURU wa Mkoa wa Mwanza Ernest Makale akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana alisema Mwansyemela alijifanya Mhandisi wa Jiji la Mwanza na alijitambulisha kwa mfanyabiashara huyo kwa jina la Alex.

Alisema baada ya kujitambulisha alimwambia ampe sh. milioni 1,000,000 amfanyie mpango wa kibali cha kuendelea kufanya biashara zake kwenye eneo hilo la hifadhi ya barabara waakti akifahamu kuwa kosa kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 15 (1a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya Namba 11/ 2007.

“Mwansyemela alianza kuomba rushwa ya shilingi milioni 1,000,000 na baadaye kutoa punguzo na kufikia makubaliano ya sh.200,000.Siku ya tukio alimtuma Mtendaji wa Kata ya Mkolani Godfrey Mwangonda (35) akampokelee kwa niaba yake na ndipo akadondokea mikononi mwa maofisa wa TAKUKURU lakini ndiye aliyefanikisha mtuhumiwa kukamatwa,” alisema Makale.

Alisema sambamba na fedha alizopokea kama rushwa kutoka TAKUKURU pia alikutwa na kiasi cha fedha zingine sh. 1,050,000 ambazo alishindwa kuzitolea maelezo alikozipata wala kufahamu kiasi cha fedha alichokuwa nacho.

Kwa mujibu wa Makale mtuhumiwa huyo alidai fedha hizo alilipwa na Barnabas Nibengo wa Mbogo Mining and General Supply ltd ambaye alikana kumpatia fedha kabla ya kubadili maelezo kuwa alipewa na mkewe ili akununue chakula cha kuku, lakini mkewe naye alikana.

“ Uchunguzi wetu fedha hizo ni rushwa kutoka kwa wananchi wengine waliotapeliwa kwani ni bayana kuwa ingawa ni mtumishi wa umma ni tapeli ambaye hafai kwenye utumishi wa umma.Kumbukumbu zinaonyesha amewahi kushitakiwa mahakamani kwa makosa ya namana hiyo,” alisema Makale .

Alieleza kuwa uchunguzi na upekuzi uliofanywa na maofisa wa TAKUKURU nyumbani kwa mtuhumiwa walimkuta akiwa na hati ya mashitaka ya kujipatgia fedha kwa njia ya udanganyifu na mashitaka ya wizi akiwa mtumishi wa umma katika kesi namba moja ya mwaka 2016.

Pia maofisa hao wa TAKUKURU wanaendelea na uchunguzi wa elimu ya mtuhumiwa huyo ingawa ana vyeti vya ufaulu mzuri kwa kidato cha nne na sita alishindwa kutoa maelezo sahihi ya elimu yake na hajui alihitimu shule gani ya sekondari wala masomo aliyosoma zaidi ya kudai alichukua mchepuo wa HGE.

Mkuu huyo wa TAKUKURU alieleza zaidi kuwa watamfikisha mahakamani leo (Ijumaa), na kueleza kuwa wananchi wengi wamekumbwa na matapeli na vitendo vya rushwa kutokana na kutafuta njia za mkato kupata ufumbuzi wa matatizo yao.

Aliongeza kuwa wananchi ni wadau wa mapambano dhidi ya rushwa, hivyo watoe ushirikiano na taarifa za vitendo hivyo TAKUKURU ili wahusika wawajibishwe kwa mujibu wa sheria, kwani serikali ipo kwa ajili yao ingawa baadhi ya watumishi wasio waadilifu wanaharibu taswira nzuri ya utumishi serikalini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...