THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Serikali Haitachukua Hatua kwa Chombo cha Habari Kinachokosoa

Frank Shija - MAELEZO.

SERIKALI imesema kuwa hakuna chombo chochote cha habari kitakachochukuliwa hatua kwa kuandika habari zenye mrengo wa kukosa sera na utekelezaji wake kama ambavyo wadau wengi wamekuwa wakiaminisha umma.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza katika Kipindi cha Habari Kuu kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Startv mjini Dodoma.

Dkt. Abbasi amesema kuwa Sheria na 12 ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 51 kinatoa ruhusa kwa chombo cha habari kukosoa kwa lengo la kuonyesha njia mbadala katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

“Hakuna chombo cha habari kitakachochukuliwa hatua kwa kukosoa, haki hiyo ipo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 51, tutaendelea kuthamini na kufanyia kazi ukosoaji huo,” alisema Dkt. Abbasi.Hata hivyo Dkt. Abbasi amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa chombo kitakachokiuka sheria na misingi ya maadili ya taaluma ya habari kwa lengo la kulinda maslahi ya taifa.

Dkt. Amesisitiza kuwa ni vyema wamiliki wa vyombo vya habari wakatumia uhuru huo wa kisheria kuchapisha habari zenye nia njema kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi badala ya kueneza hofu miongoni ya mwa jamii.

Akijibu swali la muongozaji wa Kipindi kuhusu kufungiwa kwa Gazeti la Mawio, Dkt. Abbasi amesema kuwa Gazeti hilo halijafungiwa kutokana na kuandika habari ya kukosoa Serikali isipokuwa limekiuka miiko ya taaluma kwa kuandika habari za kushushia heshima na hadhi ya mtu katika jamii pamoja na kukiuka maagizo halali ya Serikali.