THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Tanzania yafanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei Afrika Mashariki

Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

Pamoja na malalamiko na manung’uniko ya hali ngumu ya maisha kwa watanzania wengi, Tanzania ndio yenye kiwango cha chini cha mfumuko wa bei wa wastani wa asilimia 6.1 kwa mwezi Mei 2017 kwa nchi za Afrika Mashariki.

Hayo yamebainishwa leo bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2017/18.

Mhe. Dkt. Mpango amesema mfumuko wa bei katika nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka 2016 uliendelea kuwa wa kiwango cha tarakimu moja, ambapo Rwanda ilikuwa na asilimia 7.1, Uganda asilimia 5.4, Tanzania asilimia 5.2, Kenya asilimia 6.3 na Burundi asilimia 5.6.

Alisema kufikia mwezi Aprili 2017, mfumuko wa bei kwa nchi hizi ulipanda, ambapo kwa Burundi ulifikia asilimia 21.10, Rwanda asilimia 13.0; Kenya asilimia 10.28; Uganda asilimia 6.4 na Tanzania asilimia 6.4. 

“Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania mfumuko wa bei umeendelea kushuka mpaka asilimia 6.1 kwa mwei Mei 2017” amesema Dkt. Mpango

Mhe. Dkt Mpango amesema kwa miaka minne mfululizo, wastani wa mfumuko wa bei kwa Tanzania umeendelea kupungua, ukibaki katika kiwango cha tarakimu moja.

Amesema kwa mwaka 2016, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2015. Kupungua kwa wastani wa mfumuko wa bei nchini kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na: mwenendo wa kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia na nchini; kuimarika kwa upatikanaji wa vyakula nchini na hivyo kuimarisha wastani wa bei; na kuwepo kwa sera madhubuti za usimamizi wa bajeti na fedha.

Mhe. Dkt. Mpango amesema mfumuko wa bei uliongezeka kidogo, ambapo ulifikia asilimia 6.4 mwezi Aprili 2017 lakini ukiwa ndani ya maoteo ya wastani wa tarakimu moja (asilimia 5 – 8) kwa mwaka 2017.