Na Tiganya Vincent

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri  ameziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama kwa ngazi zote kuanza kuwasaka watu wanaopita pita katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwatapeli wananchi kuwa wanaweza kuwapatia fursa za Kujiunga na Jeshi la Taifa kinyume cha utaratibu uliowekwa na Jeshi hilo.

Bw. Mwanri alitoa kauli hiyo juzi Wilayani Tabora wakati akifunga mafunzo wa vijana  wa Jeshi la Kujenga Taifa Opereshi Magufuli katika Kikosi cha Jeshi cha 823 Msange JKT .

Mkuu wa Mkoa wa Tabora alisema kuwa ni vema sasa Kamati hizo kutoka chini hadi juu kuangalia kwa ukaribu taratibu zinazotumika katika kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa ili kuwabaini matapeli ambao wamekuwa wakiwalaghai wananchi na kuwatoza pesa ili wawasaidie kujiunga na Jeshi hilo, jambo ambalo ni uongo.

Awali Mkuu wa Bregedi ya 202 kundi la Vikosi vya Kanda ya Magharibi (FARU) Brigedia Jenerali Stephen Mkumbo alisema kuna haja ya viongozi wa Mkoa kushirikiana katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya taratibu za kujiunga na JKT ili kuwasaidia wasije au wasiendelee kutapeliwa fedha zao.

Alisema kuwa Makao Makuu ya  JKT wakitaka vijana wa kujiunga na Jeshi hilo wanaandika barua ya kuomba vijana na kujiunga na JKT ikiwa na masharti yanayotakiwa na kuipeleka kwenye Mikoa yote ambayo nao uandika barua ya aina ile ile na kuipeleka Wilayani nao wanashusha hadi ngazi za vijiji na sio vinginevyo.

Brigedia Jenerali huyo aliongeza kuwa mchujo uanzia ngazi za Kata na ndipo unaingia ngazi ya Wilaya na mwisho Mkoa ambapo Maafisa wa JKT uungana nao katika kuwasaili  vijana na ndipo upata wanaostahili kujiunga na Mafunzo ya Awali katika Kambi zao mbalimbali.

Alisema kuwa matapeli hao wamekuwa wakiwaibia wananchi kwa kuwatoza kuanzia shilingi laki 5 hadi milioni moja kwa madai kuwa watawasaidia kupata fursa za kujiunga na JKT jambo ambalo ni uongo na sio utaratibu unaotakiwa.

Brigedia Jenerali Mkumbo aliwaomba viongozi wa Mkoa wa Tabora kusaidia kutoa elimu juu ya utaratibu wa kujiunga na JKT ili wananchi wasaidie kuwafichua matapeli hao kwa ajili kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria .

Akisoma risala ya wahitimu wenzake 870 wa mafunzo ya awali Fred Mashauri alitoa wito wa kuongezwa kwa idadi ya vijana wa kujitolewa ikiwemo walemavu ili nao wapate fursa za kupata mafunzo ya uzalishaji mali na stadi za maisha .

Katika mafunzo hayo jumla ya wasichana 264 na wavulana 606 wametunukiwa vyeti vya kumaliza mafunzo ya awali kabla ya kwenda katika Kambi mbalimbali ili kujifunza stadi za maisha na ujarisiamali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...