Na Teresia Mhagama, DSM

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amepiga marufuku uagizaji wa nguzo za umeme, nyaya na transfoma nje ya nchi na kuliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa linanunua vifaa husika kutoka kwa wazalishaji wa ndani.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo wakati wa kikao chake na watendaji wa TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wazalishaji wa nguzo za umeme, transfoma na nyaya za umeme kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam.

Alisema kuwa kikao hicho kililenga kukutanisha pande mbili yaani REA, TANESCO na wazalishaji wa vifaa vya umeme ili kufahamu mahitaji halisi ya vifaa vya umeme na kampuni zinazotengeneza vifaa hivyo, kuieleza Serikali kama wanao uwezo wa kuzalisha vifaa husika kwa kuzingatia ubora unaohitajika.

“Tumedhamiria kusambaza umeme kwa kasi mijini na vijijini hivyo tunahitaji kufahamu uwezo wenu wa uzalishaji, tuelezeni hali halisi na kama kuna changamoto tuzijadili hapa na kufikia suluhisho kwani msimamo wa Serikali ni kutumia vifaa vya umeme vinavyozalishwa ndani ya nchi,” alisema Dkt. Kalemani.

Aliongeza kuwa ingawa Serikali imeamua kutumia vifaa vya umeme vinavyozalishwa ndani ya nchi, kampuni husika zinapaswa kuzalisha vifaa vyenye ubora ili kuiondolea TANESCO gharama ya kubadilisha miundombinu ya umeme mara kwa mara na kwamba vifaa husika viuzwe kwa gharama itakayofaidisha pande zote mbili.

Kwa upande wa mahitaji ya Transfoma, kampuni ya TANELEC, inayozalisha transfoma hizo ilieleza kuwa ina uwezo wa kutengeneza transfoma 10,000 zenye ukubwa tofauti kwa mwaka huku mahitaji ya REA na TANESCO yakiwa ni transfoma 8000 kwa mwaka hivyo watakidhi mahitaji ya hapa nchini.

Kwa upande wa kampuni inayotengeneza nyaya za umeme ya East African Cables, ilieleza kuwa ina uwezo wa kutengeza nyaya za urefu wa kilomita 14,000 zenye uwezo wa msongo wa kati (medium voltage) kwa mwaka huku mahitaji ya TANESCO na REA yakiwa ni kilomita 10,100.

Kampuni hiyo pia ilieleza kuwa ina uwezo wa kutengeneza nyaya za umeme za urefu wa kilomita 38,000 zenye uwezo wa msongo wa chini (low voltage) huku mahitaji ya REA na TANESCO yakiwa ni kilomita 31,000 kwa mwaka hivyo itaweza kukidhi mahitaji ya nyaya hizo nchini.

Kuhusu uwezo wa wazalishaji wa nguzo nchini, kampuni zilizohudhuria kikao hicho zilieleza kuwa zina uwezo wa kuzalisha nguzo takribani 1,200,000 kwa mwaka huku mahitaji ya TANESCO na REA yakiwa ni nguzo 1,000,000 kwa mwaka.

Dkt. Kalemani alitoa wito kwa kampuni hizo za Tanzania kuhakikisha kuwa wanatekeleza mahitaji ndani ya wakati na viwango vinavyokubalika ili kuweza kuhakikisha kuwa Sekta ndogo ya Umeme inaivusha nchi kwenda uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
 Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kushoto) akiwa katika kikao na watendaji wa TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wazalishaji wa nguzo za umeme, transfoma na nyaya za umeme kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam.
 Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo ( wa kwanza kushoto) akiwa katika kikao na  watendaji wa TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wazalishaji wa nguzo za umeme, transfoma na nyaya za umeme kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni  Kaimu Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga (wa pili kushoto),  Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Dkt. Gideon Kaunda (wa tatu kushoto) na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa  TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.
Baadhi ya wazalishaji wa nguzo za umeme, transfoma na nyaya za umeme wakiwa katika kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam ambacho kiliongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...