Na Greyson Mwase, Geita
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, ametoa siku 13 kwa mameneja wote wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha wananchi wote waliolipa ada kwa ajili ya kuunganishiwa huduma ya umeme wanaunganishiwa mapema na kuondokana na adha ya kuwepo gizani.
Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo katika kijiji cha Nyijundu wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wakati akizindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu kwa mkoa wa Geita pamoja na kumtambulisha mkandarasi atakayetekeleza mradi kwa mkoa huo.
Alisema kuwa, ni haki ya mwananchi aliyelipia gharama za kuunganishiwa umeme kupatiwa huduma ndani ya siku saba kama sheria inavyofafanua na kuwataka mameneja kuhakikisha wananchi wote waliokuwa wamelipia huduma za kuunganishiwa umeme kupata huduma hiyo kabla ya Julai 25, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani aliwataka mameneja wa TANESCO kusogeza huduma karibu na wananchi badala ya wananchi kusafiri umbali mrefu kwa gharama kubwa kufuata huduma za umeme.
Alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuinua uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha nishati ya umeme ya uhakika inapatikana hususan katika maeneo ya vijijini ili wananchi waweze kujiajiri kupitia viwanda vidogo vidogo kama mashine za kusaga na kukoboa nafaka, kuchomelea vyuma na kusindika matunda.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga akielezea hali ya upatikanaji wa umeme katika mkoa huo mbele ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kwenye uzinduzi huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko akifafanua jambo kwenye uzinduzi huo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akitoa maelekezo kwa wakandarasi na watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) (hawapo pichani) kwenye uzinduzi huo.
Sehemu ya wakandarasi na watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakipokea maelekezo kutoka kwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kwenye uzinduzi huo.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani akitoa sehemu ya vifaa maalum vya Umeme Tayari (UMETA) kama zawadi kwa sehemu ya wazee wa kijiji cha Nyijundu wilayani Nyang’hwale kwenye uzinduzi huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...