Na Hyasinta
Kissima, Njombe
Halmashauri ya Mji Njombe
imerudisha heshima yake kwa kupata Hati safi katika ripoti ya mthibiti na
mkaguzi wa serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2015/2016) ambapo kwa mwaka wa
fedha 2014/2015 Halmashauri hiyo ilipata hati inayoridhisha na yenye maswala ya
msisitizo.
Akitoa mapendekezo yake
wakati wa Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani la kujadili hoja za Mthibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Jackson Saitabahu ameipongeza Halmashauri kwa
kupata hati safi na kwa kukusanya mapato kwa asilimia 100.1 na amezitaka idara
na vitengo vya Halmashauri kutoona Ofisi ya Ukaguzi wa ndani kama mwiba wa pori
na mahali pasipoingilika kwani Kitengo hicho kipo kwa ajili ya kutoa ushauri
lakini pia kuiandaa Halmashauri kwa Ukaguzi Mkuu hivyo wasisite kuomba ushauri
pale inapobidi.
“Hati safi haiji kwa bahati
mbaya, napenda niwapongeze kwa jitihada kubwa mlizoonyesha lakini pia niwasihi
sana msikwepe Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani, Kitengo hiki kinatakiwa kiwezeshwe
vizuri na Halmashauri ijenge mahusiano mazuri na Kitengo cha Ukaguzi kwani
wakaguzi wa ndani ndio wanatuandaa kwa ajili ya ukaguzi wa nje.Tunapoimarisha
mahusiano mazuri miongoni mwetu hatutakua na hoja za ukaguzi.Tusiwe mabingwa wa
kujibu hoja zaidi ya kuwa wataalamu wa kuzuia hoja zisitokee.”Alisema Katibu
Tawala.
Sambamba na hilo
Halmashauri pia imeendelea kuimarika kwa kufikia asilimia 35% za kuweza
kujitegemea jambo ambalo limeendelea kuifanya Halmashauri ya Mji Njombe kufanya
vizuri katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa mwaka 2017/2018 Halmashauri
imejipanga kuhakikisha kuwa hoja zote zinafungwa, kukusanya mapato zaidi ya
mwaka uliopita na kuhakikisha kuwa Halmashauri haitoruhusu kufanya biashara na
Wakandarasi na wazabuni wasio na mashine za kielektroniki na kuhakikisha kuwa
nyaraka na kumbukumbu zote za manunuzi zinatunzwa ipasavyo.
Mweka Hazina wa Halmashauri ya Mji Njombe Dorcas Mkello akiwasilisha hoja za ukaguzi mbele ya Mkutano Maalumu wa Baraza Kuu la Madiwani.
Wakuu wa Idara na Vitengo Halmashauri ya Mji Njombe wakisikiliza kwa Makini mapendekezo ya Baraza la Madiwani.
Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Jackson Saitabahu akitoa mapendekezo yake mara baada ya kupitia hoja za ukaguzi.
Madiwani wakipitia makabrasha yenye hoja za Ukaguzi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...