Na Karama Kenyunko-Globu ya Jamii.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeambiwa kuwa, mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Power African Power (T) Limited (PAP) ambaye pia ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha, Harbinder Singh Sethi ni mgonjwa sana na anasumbuliwa na uvimbe tumboni.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Wakili wa mshitakiwa, Alexi Balomi ambaye amedai mahakamani hapo kuwa, hali ya mteja wake Seth imekuwa ikibadilika kwa wiki nne sasa na kwamba imezidi kuwa mbaya kwa kuwa hawezi kupata usingizi na hivyo anahitaji uangalizi wa madaktari..

Kabla ya hoja hiyo ya ugonjwa, Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi Mwendesha Mashitaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai alidai kuwa kesi hiyo ilikuja kwa kutajwa na upelelezi bado haujakamilika.

Balomi amedai kuwa kutokana na hali mbaya ya mteja wake Seth,wamebahatika kupata nyaraka kadhaa kutoka kwa daktari kwani Hata siku aliyokamatwa alikuwa akienda kwenye matibabu Afrika Kusini alisema huku akitaka kutoa nyaraka hizo.

Hata hivyo, Swai alidai nyaraka ambazo Wakili Balomi anataka kuziwasilisha mahakamani hapo kuhusiana na Sethi hazijakidhi vigezo vya sheria na kwamba alitegemea daktari ambaye anamtibu angefika mahakamani kueleza hali halisi ya ugonjwa husika.

Akijibu hoja hiyo, Hakimu Shaidi amesema suala la ugonjwa siyo la kufumbiwa macho, linapaswa kuchukuliwa kwa uzito na kuelekeza magereza kufanya kila linalowezekana kuhakikisha hali ya mshitakiwa huyo inakuwa nzuri na ikibidi, wawasiliane na wataalam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuhakikisha mshitakiwa anapohitajika mahakamani anafika kama inavyotakiwa.

Kesi imeahirishwa hadi Julai 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Seth anashtakiwa pamoja na James Rugemarila ambaye ni Mkurugenzi wa VIP Engineering na mmiliki mwenza wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL), ambao wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani milioni 22. 1 na Sh bilioni 309 pamoja na utakatishaji fedha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...