Na Joachim Mushi wa TBN
Kampuni ya Jamii Media ya Tanzania inayoendesha mitandao ya JamiiForums na FikraPevu kwa kushirikiana na CIPESA(The Collaboration on International ICT Policy in East and Southern Africa) iliyo na makao makuu yake nchini Uganda imefanya Kongamano la kuwakutanisha wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) nchini hasa wanaohusika moja kwa moja katika kulinda faragha za wateja wao ili kujadili masuala mbalimbali ya Huduma za Habari na Mawasiliano katika jukumu lao kuwa kiunganishi kati ya mteja na huduma watoazo pamoja na namna ya kulinda usiri wa taarifa za wateja wanaotumia huduma hizo.

Kabla ya kufanyika kwa Kongamano hilo siku ya Jumatano tarehe 12 Julai, Jamii Media ilifanya mafunzo ya siku mbili kuanzia tarehe 10 hadi 11 Julai kwa vijana mbalimbali wakiwemo wanasheria, wanaharakati na wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Mafunzo hayo yalilenga kujenga uelewa kuhusu sera zinazohusu Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Usalama wa Data Mtandaoni, Hali ya Uhuru Mitandaoni na Mambo yanayoathiri uhuru Mitandaoni nchini Tanzania.

Katika Kongamano hilo, Mwakilishi wa Jeshi la Polisi Tanzania, Dawson Msongaleli kutoka kitengo cha Makosa ya Mtandaoni alifanya pia Uwasilishaji kuhusu Sheria ya Makosa Mtandaoni na kueleza kuwa Usiri na Usalama wa taarifa za watumiaji wa mtandao ni vitu viwili vinavyokanganya na kwamba inafika wakati ili kutekeleza kimoja inabidi misingi ya kingine ivunjwe.

Aidha, alibainisha kuwa kukosekana kwa kanuni za usimamizi wa Sheria ya Makosa ya Mtandao (The Cyber Crimes Act, 2015) ni changamoto kubwa kwani inapelekea tafsri ya Sheria hiyo kubadilika kulingana na mazingira na mtu anayetafsiri kitu ambacho kinaathiri kazi yao kama watekelezaji wa Sheria na kuahidi kuwa mamlaka zinashughulikia chamgamoto hiyo.

Mara baada ya kumalizika kwa kongamano hilo, Mkurugenzi wa Jamii Media, Bw. Maxence Melo alisema hili ni Kongamano la kwanza la aina hii kufanyika tangu kuanzishwa kwa JamiiForums miaka 11 iliyopita na limekuwa na matokeo chanya baada ya wadau kujadili kwa kina masuala mbalimbali yahusuyo usalama wa watumiaji. Aliongeza kuwa wadau wengi kwenye kongamano hilo wameunga mkono hatua ya uwekaji wa sheria za kusimamia huduma nzima ya matumizi ya mitandao lakini wakashauri ufanywe kwa kutoa fursa za maendeleo na si kuminya ubunifu wala uhuru na usiri wa watumiaji wa huduma hizo.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa kampuni yake itaendelea kutoa mafunzo kwa wadau mbalimbali wa huduma za mawasiliano wakiwemo wamiliki wa blogu na watumiaji wa kawaida wa mitandaonya kijamii ili kuhakikisha wanakuwa na matumizi mazuri ya huduma hiyo ili kupunguza mkanganyiko kwao na kuwapa fursa adhimu ya kunufaika na uwepo wa mitandao hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Mello (wa pili kulia) akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kumalizika kwa kongamano la wadau wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) nchini Tanzania, lililoandaliwa na Kampuni ya Jamii Media ya Tanzania wamiliki wa mitandao ya Jamii Forums na Fikra Pevu kwa kushirikiana na Kampuni ya CIPESA ya nchini Uganda. Wengine ni Mkurugenzi wa CIPESA, Dk. Wairagala Wakabi (wa kwanza kulia) na Kutoka kushoto ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya Jamii Media, Asha Abinallah na Mkurugenzi wa Jamii Media, Mbaraka Islam. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...