THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

MAKALA YA SHERIA: KAMA HAIJAPITA MIAKA 12 UNAWEZA KURUDISHA ARDHI ULIYODHULUMIWA.

Na  Bashir   Yakub
1.UKOMO  WA  HAKI.
Hakuna  haki  isiyo  na  ukomo wa  muda  unapokuwa  unaidai. Huwezi  kudai  haki  muda  wowote  unaotaka  wewe. Ni  lazima   udai  haki  ndani  ya  muda.Na  ni  ule  muda tu uliowekwa  na  sheria. Ipo  sheria  rasmi  inayoeleza  muda  wa  kudai  haki  mbalimbali.  Inaitwa Sheria  ya  Ukomo  wa  Muda ,  Sura  ya  89.  Katika  sheria  hiyo   hapajaelezwa tu   ukomo  wa  kudai  haki  katika  masuala  ya  ardhi  bali  pia  katika  masuala  mengine  yote  ya  haki  unazoweza  kudai.
Ndani  ya  Sheria  ya  Ukomo  wa  Muda  kumeelezwa ukomo  wa  kudai  haki  iliyotokana  na  masuala  ya  mikataba na  makubaliano, ukomo   wa  kudai  haki  katika  masuala  ya  udhalilishaji, ukomo  wa rufaa, ukomo  wa  haki  katika  masuala  ya bima, madai  ya  fedha,  rehani  za  mikopo, na mambo  mengine  mengi.

2.  HUJAPITWA  NA  MDA  BADO UNAWEZA  KUIDAI  ARDHI  YAKO.
Wako  watu  huko  nyuma  walidhulumiwa  ardhi  muda  mrefu  na  sasa  wamekata  tamaa.  Wamekata tamaa  kutokana  na  kuona   ni mda  mrefu  umepita  tangu  haki  hiyo  iporwe  na  sasa  wanadhani  kuwa   hawawezi  tena  kudai  haki  hiyo.
Wako  watu wamedhulumiwa  ardhi  katika  masuala  ya  mirathi,  katika  masuala  ya  mikopo,  katika  masuala  ya  mikataba  na  makubaliano,  katika  masuala  ya  ndoa  na  machumo  ya mali  za  ndoa, katika  masuala  ya  uvamizi, katika  masuala  ya  kuharibu  mipaka  n.k. Na  ardhi  hapa  tunazungumzia  mashamba,  viwanja  na  nyumba. Hivi  kwa  pamoja  ndivyo  huitwa  ardhi.
Basi  yafaa  ujue  kuwa kama  wewe  ni  kati  ya  waathirika  wa  jambo  hili  basi  bado unayo  haki  ya  kudai   ardhi  yako  madhali  muda  huo  haujakupita.  Haki  yako  inaishi   mpaka  miaka  12  na  itakufa baada  ya  muda  huo.  Kama  imepita  miaka  sita,  mitano,  nane,  kumi,  n.k.  bado  muda  wako  wa  kudai  na  kurudishiwa  ardhi upo.