Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewasili usiku huu Jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo hapo kesho tarehe 03 Julai 2017 atahudhuria Mkutano wa 29 wa Wakuu wa  Nchi na Serikali  wa Umoja wa Afrika (AU).

Katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole Jijini Addis Ababa Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amepokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Ethiopia Pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Naimi Aziz na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Augustine Mahiga.

Katika Mkutano huo wa siku mbili kuanzia tarehe 03-hadi 04 Julai-2017, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan atamuakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwenye mkutano huo.

 Kabla ya ufunguzi rasmi, Mkutano huo ulitanguliwa na vikao vya Baraza la Utendaji linalowashirikisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Kamati ya Uwakilishi wa Kudumu  inayowahusisha Makatibu Wakuu wa Wizara za Mambo ya Nje kutoka nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika.

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi  na Serikali  utafunguliwa rasmi kesho tarehe 03-Julai-2017 katika Makao Makuu ya Umoja wa Afrika Jijini Addis Ababa, Ethiopia na  utajikita katika kujadili masuala mbalimbali yanayohusu umoja huo.

Miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na taarifa  kuhusu Maboresho katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na maboresho ya kitaasisi katika AU na  hali ya Ulinzi na Usalama katika bara la Afrika.

Kuhusu  hali ya  ulinzi na usalama katika Bara la Afrika majadiliano ya Viongozi hao yatajikita zaidi kwenye nchi za Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo- DRC na Libya.  Aidha, majadiliano hayo pia yatagusa  hali ya usalama kwenye baadhi ya nchi ambazo ziliathiriwa na kundi la Boko Haram za  Nigeria, Niger, Chad na Cameroon.

Mkutano huo 29 wa AU, unatarajiwa kuhuduhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas.

Mkutano huo 29 wa AU utakaofanyika Jijini Addis Ababa, Ethiopia utaongozwa na Mheshimiwa  Alpha Conde  Rais wa Jamhuri ya Guinea ambaye ndiye Mwenyekiti wa AU.

Kauli Mbiu ya Mkutano huo ni Kuimarisha Mgawanyiko wa Idadi ya Watu Kupitia Uwekezaji katika Vijana (Harnessing Demographic Divident Through Investments in the Youth)

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
 ADDIS ABABA- ETHIOPIA.      

03-Julai-2017
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amewasili usiku huu Jijini Addis Ababa, Ethiopia ambapo hapo kesho tarehe 03 Julai 2017 atahudhuria Mkutano wa 29 wa Wakuu wa  Nchi na Serikali  wa Umoja wa Afrika (AU).Mhe.Samia amepokelewa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Ethiopia Pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Naimi Aziz na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Augustine Mahiga.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt Augustine Mahiga mara baada ya kuwasili jijini Addis Ababa,nchini Ethiopia usiku huu.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassa akizungumza jambo na Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania,Dkt Jakaya Kikwete mara baada ya kuwasili jijini Addis Ababa mapema usiku huu

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...