Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amezindua huduma mpya ya fedha mtandao ijulikanayo kama TTCL PESA ya Kampuni ya Simu Tanzania TTCL. Uzinduzi huo umefanyika katika Makao Makuu ya TTCL barabara ya Samora jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mheshimiwa Omari Nundu ambaye ni Mwenyeketi wa Bodi ya TTCL, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujezi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Anjelina Madete, Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Bwana Waziri Kindamba, Wajumbe wa Bodi na wafanyakazi wa TTCL.

Akizungumza katika hafla hiyo Makamu wa Rais alisema uzinduzi wa huduma ya TTCL PESA ni mwendelezo wa jitihada za Kampuni hiyo kurejea katika nafasi yake ya awali ya kuwa suluhisho la kweli la utoaji huduma za Mawasiliano hapa nchini.

“Kuzinduliwa kwa huduma hii ni uthibitisho mwingine kwamba, TTCL inatekeleza kikamilifu maagizo ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu mpendwa Dkt John Pombe Magufuli ambaye ameelekeza kuwa, Mashirika yote ya Umma yajiendeshe kwa faida, yatoe gawio Serikalini, yawahudumie wananchi kwa kiwango cha juu kabisa cha ubora na kwa gharama nafuu” alisema Makamu wa Rais.

Aidha, Makamu wa Rais alisisitiza kwamba TTCL PESA itawezesha wananchi kutuma na kutoa pesa kwa viwango vya chini kabisa kupita mitandao yote, pia itawezesha wananchi kulipia Bill za Umeme (LUKU), Maji, Ving’amuzi na kuwezesha wateja kununua muda wa maongezi na vifurushi vya data vya TTCL. Aliwataka TTCL kuendelea kuwa wabunifu zaidi ili waweze kuongeza huduma nyingine kadiri mahitaji na siku zinavyokwenda.

Akijibu kuhusu changamoto zilizotajwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Makamu wa Rais alisema Serikali inazijua na itaendelea kuzipatia majawabu. Hatahivyo aliwataka watumie vyema rasilimali walizopewa ikiwamo Mkongo wa Taifa na Kituo cha Kuhifadhia Kumbukumbu za kimtandao kupata pesa za kujiendeshea.

Makamu wa Rais pia aliipongeza menejimenti ya TTCL kwa wazo lao la kufikiria kuanzisha kiwanda cha simu hapa nchini. Alisema “msisitizo wa serikali yetu kwa sasa ni ujenzi wa uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025 kupitia uwekezaji katika viwanda hivyo wazo lenu la ujenzi wa kiwanda cha simu limekuja wakati muafaka”.

Mwisho, Makamu wa Rais alisema TTCL PESA itatoa fursa kubwa ya ajira kwa wananchi kuwa mawakala na itarahisisha shughuli za kiuchumi hasa biashara na hivyo aliwasihi wananchi kuonesha uzalendo wao kwa kutumia huduma za TTCL.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akivuta pazia kuashiria uzinduzi wa huduma ya TTCL Pesa uliofanyika Makamu Makuu ya TTCL barabara ya Samora jijini Dar es Salaam, kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Ndugu Wazir W. Kindamba. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akivuta pazia kuashiria uzinduzi wa huduma ya TTCL Pesa uliofanyika Makamu Makuu ya TTCL barabara ya Samora jijini Dar es Salaam. 
Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Ndugu Wazir W. Kindamba (kulia) akimuonesha namna ya kutumia huduma ya TTCL Pesa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mara baada ya kukamilika kwa uzinduzi wa TTCL Pesa uliofanyika Makamo Makuu ya TTCL barabara ya Samora jijini Dar Es Salaam. 
Afisa Mtendaji Mkuu wa TTCL Ndugu Wazir W. Kindamba (katikati) pamoja na Mwenyekiti ya Bodi ya TTCL Mhe. Omari Nundu wakimuonesha kwa vitendo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan jinsi pesa inavyotumwa na kupokelewa kupitia huduma ya TTCL Pesa mara baada ya kukamilika kwa uzinduzi wa TTCL Pesa uliofanyika Makamo Makuu ya TTCL barabara ya Samora jijini Dar Es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Mimi binafsi nafikiri TTCL kama TANESCO wanashindwa kutambua nafasi yao kibiashara na kuona fursa.

    Mfano katika biashara ambayo TANESCO wapo naamini kama kampuni tanzu ya serikali ingejikita zaidi katika kitu kimoja tu: TRANSMISSION yaani kujenga miundo mbinu kati ya uzalishaji (GENERATION) na ugawaji/ kwa walaji (DISTRIBUTION). Kimsingi kazi ya kuzalisha na ugawaji waache kwa wajasiliamali wafanye.

    Namna hiyo hiyo TTCL inabidi iache kufanya kazi kana kwamba wao ni Halotel, wafikirie makubwa zaidi katika kuwezesha makampuni kama Halotel kuongezeka na kwa minajidili hiyo kuongeza ajira nyingi zaidi. Sioni kama taifa lilikuwa linahitaji namna moja zaidi ya kutuma fedha kwa simu!

    Hayo ni mawazo yangu, yanaweza kuwa finyu kwamba makampuni ya serikali yawe mabunifu zaidi, si mambo ya kuburuza (photocopying) tu na kushindana na walipa kodi wadogo wadogo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...