Kampuni  ya Moovn Technologies kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania PLC, wamezindua ushirikiano mpya utakaowarahisishia wateja wao kupata huduma ya usafiri na kuwafikishia huduma za simu watu zaidi ya milioni 12 barani Afrika.


Moovn ni teknalojia inayomwezesha mtu anayetaka usafiri kuupata kwa haraka akiwa sehemu alipo kwa kutumia simu yake ya mkononi au kompyuta. Teknalojia hii pia inawawezesha watu kufikishiwa bidhaa kutoka sehemu mbali mbali na madereva.


Ushirikiano huu kati ya Vodacom ambayo ni moja kati ya makampuni makubwa ya simu za mkononi Afrika pamoja na Moovn, utawawezesha watu zaidi ya milioni 12 kujiunga kwenye huduma hiyo ya Moovn app kwa kupitia simu zao za mkononi.


Kupitia mpango huo, kampuni ya Vodacom itatoa bure au kwa punguzo huduma za data kwa wateja wa Moovn pamoja na madereva ili waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.



Wateja wa huduma hiyo wataweza  kuchagua usafiri wa aina mbali mbali kama vile boda boda, bajaji pamoja na taxi kulingana na mahitaji yao kwa kutumia Moovn app. Pamoja na kulipa kwa fedha taslimu, wataweza pia kulipa kwa kutumia huduma ya kifedha ya M-Pesa



Huduma hii ya aina yake inalenga kuboresha maisha ya wateja wa kampuni zote mbili zilizo kwenye ushirikiano. Ushirikiano huu pia unalenga kutengeneza ajira pamoja na kuboresha hali ya kiuchumi kwa jamii za Kitanzania na Afrika kwa ujumla.



“Tunayo furaha kuungana na mshirika mwenzetu katika kutoa huduma hii muhimu tukilenga kwa pamoja  kubadili maisha ya watu,” anasema Godwin Gabriel ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Moovn



Kumhakikisha mteja usalama wake, mtumiaji wa huduma hii anaweza kubonyeza batani inyoitwa ‘panic button’ na ujumbe mfupi wa maandishi utatumwa kwa mtu wake wa karibu ukieleza sehemu alipo na utambulisho wa dereva muda wowote wakati akiwa kwenye chombo cha usafiri.



Kipengele hiki cha usalama ni muhimu kwa kuwa kwa siku za hivi karibuni kumekuwa  na matukio ya abiria kufanyiwa uhalifu na baadhi ya madereva wasio waaminifu. Mteja pia anaweza kuwafamisha ndugu jamaa na marafiki zake kinachoendelea kuanzia mwanzo hadi mwisho wa safari yake.



Pamoja na mambo mengine, huduma hii itawawezesha wafanyabiashara kufuatilia bidhaa na huduma wanazowapelekea wateja wao kuanzia wanapomkabidhi dereva hadi zinapomfikia mteja.



Madereva  watakuwa wakipata malipo yasiyobadilika (Flat commission) kwa kila safari watakokuwa wakifanya na  kwa upande wao wateja watafurahia gharama zisizopanda.



Naye Mkurugenzi wa kitengo cha biashara wa Vodacom Hisham Hendi alisema “M-Pesa inawawezesha watu wote kuweza kufikiwa na huduma ya kifedha kwa urahisi katika sehemu walipo. Wakati tukifanya kazi kubwa kuhakikisha kuwa watanzania wengi wanafikiwa na huduma za gharama nafuu za kifedha, tunaendelea pia kuwaletea wateja wetu huduma zenye ubunifu zinawezesha Serikali na biashara kuwasiliana huku tukitoa malipo mazuri kwa mawakala wetu,”



Aliwashauri watumiaji wa mtandao huo kwa kufanya malipo kwa njia ya simu kwani ni salama zaidi kuliko kubeba fedha taslimu. Kupitia huduma ya LIPA KWA M-PESA alisema malipo katika huduma nyingi na bidhaa yamerahisihwa kupitia App mpya ya M-Pesa

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...