NA EVELYN MKOKOI –MASWA 

Naibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na mazingira Mhe. Luhaga Mpina, amewapongeza viongozi wa mikoa wilaya na halmashauri nchini waliotekeleza kwa kiwango cha kuridhisha agizo la kusimamia utekelezaji wa siku ya kitaifa ya kufanya usafi na kuhakikisha usafi wa mazingira katika maeneo yao unaimarishwa.

Mpina ameyasema hayo leo Wilayani Maswa alipokuwa akishiriki zoezi la kufanya usafi kitaifa na kuongeza kuwa majina ya viongozi hao pamoja na wale ambao wamezembea kutekeleza agizo hilo yatafikishwa kwa Mhe. Rais na Mhe. Makamu kwa hatua za kiutendaji.

“Hatuwezi kufikia mapinduzi ya uchumi wa viwanda kama taifa litaendelea kuwa chafu kwani tutaendelea kupoteza nguvu kazi nyingi kutokana na maradhi yanayosababishwa na uchafu, hivyo viongozi wa mikoa na wilaya wana jukumu kubwa la kusimamia usafi wa mazingira.” Alisisitiza Mpina.

Naibu Waziri Mpina aliongeza kwa kusema kuwa serikali imeona kuwa usafi ndio afya na usafi ndio maisha na ndio maana Serikali imeitenga siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa ni siku maalum kwa ajili ya usafi wa Mazingira. 

Akiwa ziarani wilayani Maswa Mhe. Mpina alibaini changamoto mbalimbali za kimazingira zinazoikumba wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na upungufu wa matundu ya vyoo katika soko la Maswa, mazingira yasiyoridhisha ya kufanyia biashara sokoni na ukosefu wa maji katika machinjio ya wilaya, ambapo aliekeza uongozi wa Halmashauri kuhakikisha ndani ya miezi mitatu changamoto ya upungufu wa matundu ya choo iwe imefanyiwa kazi, kuwepo kwa mabanda ya kisasa ya kufanyia biashara katika soko hilo na kuhakikisha kunakuwepo na maji ya kutosha wakati wote katika machinjio.

Kwa Upande wake kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa Bw. Vivian Christopher, alieleza kuwa Halmashauri yake imetenga fedha kwa ajili ya kushughulikia changamoto hizo katika Bajeti wilaya kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
Pichani Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Luhaga Mpina Akizungumza na Baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya Wilaya wa Maswa (hawapo katika picha)  leo baada ya kukamilika kwa zoezi la usafi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...