Benny Mwaipaja, WFM, DAR ES SALAAM

SERIKALI ya Norway imeipatia Tanzania msaada wa Dola Milioni 10.5 za Marekani kupitia programu ya miaka mitatu ya maboresho ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, inayotarajiwa kuanza Mwaka Mpya wa Fedha- Julai Mosi mwaka huu.

Mpango huo pamoja na uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Mafuta, umezinduliwa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Borge Brende, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Dkt. Juliana Pallangyo kwa niaba ya Serikali zao.

Dkt. Mpango ameishukuru Serikali ya Norway kwa msaada huo mkubwa utakaochangia kuboresha utendajikazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa kuijengea uwezo zaidi wa kitaalamu, miundombinu na vitendeakazi vingine vitakavyo changia kuongeza uwezo wa Mamlaka hiyo wa kukusanya mapato ya Serikali.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Dkt. Juliana Pallangyo amesema kuwa hatua ya Serikali ya Norway kuendelea kufadhili programu ya pili ya Mpango wa kuendeleza Sekta ya Mafuta utaiwezesha Serikali kubobea katika masuala ya utaalamu wa masuala ya sheria na usimamizi wa sekta hiyo.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway, Mhe. Borge Brende amesifu utendaji kazi mahili wa Mhe. Rais Dokta John Pombe Magufuli wa kupambana na ufisadi na vitendo vya rushwa pamoja na kuimarisha ukusanyaji kodi, hatua ambayo itaifanya nchi ipige hatua za maendeleo haraka.

Amesema kuwa hajawahi kuona nchi yoyote duniani ikiendelea bila kuweka nidhamu na uwajibikaji serikali pamoja na kutokusanya mapato yake ipasavyo na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya tano kufanikisha mipango yake ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) na Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Borge Brende wakielezana jambo kabla ya kuzindua rasmi Mpango wa miaka mitatu wa Maboresho ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na uzinduzi wa awamu ya pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Mafuta, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Borge Brende akielezea kuhusu kuendelea kwa ushirikiano wenye tija na Tanzania wakati wa kuzindua rasmi Mpango wa Maboresho ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na uzinduzi wa awamu ya pili ya program ya maendeleo ya Sekta za Mafuta jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akizungumza jambo wakati wa kuzindua rasmi Mpango wa miaka mitatu wa Maboresho ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na uzinduzi wa awamu ya pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta za Mafuta, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia), Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Borge Brende (katikati) na Balozi wa Norway nchini Tanzania Hanne Marie Kaarstad wakimsikiliza Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Dkt. Juliana Pallangyo (hayupo pichani) wakati akielezea umuhimu wa Program ya Maendeleo ya Sekta za Mafuta, Jijini Dar es Salaam.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...