· Yaanza kuuza makaa hayo kwa kasi
· Yakiri kuwa na akiba ya makaa ya mawe ardhini ya kuchimba kwa zaidi ya miaka mia moja. 

Na Koleta Njelekela-STAMICO

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza rasmi kuuza makaa ya mawe yanayozalishwa katika Mgodi wake wa Kabulo ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wakiwemo viwanda vya saruji na nguo na hivyo kukuza Pato la Taifa.

STAMICO ilianza uzalishaji wa majaribio wa makaa ya mawe katika mgodi wa Kabulo uliopo Kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe mnamo tarehe 30 Aprili 2017 na mpaka sasa imeweza kuzalisha tani 6,197.

Akihojiwa na Mwandishi wa Habari hii, mara baada ya zoezi la uuzaji makaa ya mawe kuanza rasmi huko Kabulo jana (6 Julai 2017), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Bwana Hamis Komba, amesema Shirika kupitia mradi wake wa makaa ya mawe wa Kabulo, sasa linaweza kukidhi mahitaji ya watumiaji wote wa makaa ya mawe nchini, katika kipindi cha miaka mia mfululizo kutokana na kuwepo kwa mashapo ya kutosha (mineral resources) na nyenye ubora wa juu katika mgodi huo.

Bwana Komba amesema matarajio ya Shirika ni kuongeza kiwango cha uchimbaji makaa ya mawe kutoka tani 600 hadi tani 1000 kwa siku, hatua ambayo itaiwezesha STAMICO kuzalisha zaidi ya tani 300,000 kwa mwaka. 

“Nchi yetu ina rasilimali nyingi za madini yakiwemo makaa ya mawe, hivyo tunapenda kuwahikishia wenye viwanda vinavyotumia makaa hayo hususani viwanda vya Saruji (Cement), kwamba nchi ina makaa ya kutosha hivyo Serikali haitoshindwa kutosheleza mahitaji na makaa yam awe huku ikitekeleza kwa vitendo azma yake kujenga Tanzania yenye viwanda, ili kukuza uchumi wa Taifa" Alifafanua Bwana Komba.
Kamishna wa Madini Tanzania Mhandisi Benjamin Mchwampaka akiwa katika picha ya pamoja na timu wa wataalam wa STAMICO (wanaotekeleza Mradi wa Uchimbaji Makaa ya Mawe-Kabulo) alipotembelea Mgodi huo hivi karibuni kukagua maendeleo ya mradi huo ambao ulianza rasmi uzalishaji makaa yam awe tarehe 30 Aprili, 2017 na kufanikiwa kuzalisha tani 6197 mpaka sasa. Soko la ndani la makaa hayo linawalenga wazalishaji viwandani hususani wale wa viwanda vya Saruji (Cement) na watengenezaji wa nguo, pamoja na magereza na watumiaji wengine wa majumbani.

Shughuli za Uchimbaji Makaa ya Mawe zikiendelea katika mgodi wa Kabulo Kiwira, uliopo katika Kijiji cha Kapeta, wilaya ya Ileje, Mkoa wa Songwe. Leseni za Uchimbaji wa Awali wa Madini katika eneo hilo la Kabulo, zina zaidi ya tani milioni 35 zilizothibitishwa za mashapo ya makaa ya mawe, yaliyoko karibu na uso wa ardhi, katika mgodi huo wa Kabulo. Mashapo hayo yanaweza kuchimbwa kwa mfululizo kwa miaka mia moja ijayo.

Mratibu wa Mradi wa Uzalishaji Mkaa ya Mawe wa Kabulo-Kiwira Bwana Alex Rutagwelela ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji wa STAMICO akielekeza kuhusu zoezi zima la upakiaji makaa ya mawe katika Malori tayari kwa ajili ya kupeleka katika eneo la mauzo lililopo katika kijiji cha Kasumulu, Wilaya ya Kyela, mkoa wa Mbeya. Mgodi huo wa Kabulo-Kiwira uliopo katika kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe unamilikiwa na kuendeshwa na STAMICO kwa niaba ya Serikali.
Malori ya Kampuni ya Lake Cement yakipakia Makaa ya Mawe katika eneo la mauzo ya makaa hayo, lililopo umbali wa kilometa mbili kutoka katika barabara kuu ya Mbeya, iendayo nchini Malawi. Eneo hilo la mauzo lipo katika kijiji cha Kasumulu, Wilaya ya Kyela, mkoa wa Mbeya. Makaa hayo ya Mawe yanazalishwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), katika mgodi wake wa Makaa ya Mawe wa Kabulo, ulipo katika kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje mkoa wa Songwe.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...