Tanzania imesisitiza uamuzi wake wa kuendelea na mpango wa kujenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler's Gorge Hydro Power Project) yaliyopo ndani ya Pori la Akiba la Selous mbele ya wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia kutokana na umuhimu wake kwa maendeleo ya Watanzania.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika mkutano wa 41 wa wajumbe wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaoendeshwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ambao unaendelea katika Jiji la Krakov nchini Poland, Kiongozi wa msafara huo ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo kuwa mpango huo ulikuwepo katika ajenda ya Serikali ya Tanzania tangu miaka ya 1960's na kwamba ukubwa wa eneo litakalotumika kutekeleza mradi huo ni asilimia tatu tu ya eneo lote la pori hilo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 50,000.

Aliongeza kuwa, “Itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 1982 wakati pori hili (Selous) limewekwa katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhifadhi wa Asili (IUCN) liliutambua mradi huo wa Stiegler's Gorge kutokuwa na madhara makubwa katika uharibifu wa mazingira ukizingatia ukubwa wa pori hilo na eneo litakalotumika kujenga mradi huo”.

Aliwaeleza wajumbe hao kuwa, Serikali ya Tanzania inatekeleza sera ya kujenga uchumi wa viwanda hali inayopelekea kuwa na mahitaji makubwa ya nishati ya umeme hivyo kwa kuzingatia vyanzo vilivyopo imekuwa ni muhimu sasa kufikiria tena ujenzi wa mradi huo kama chanzo kingine muhimu cha nishati kuwezesha kufikia azma hiyo.

Alisema mradi huo utaongeza uzalishaji wa umeme nchini kufikia asilimia 144.8 hivyo kuondoa upungufu wa nishati uliopo kwa sasa na pindi utakapokamilika utawanufaisha watanzania wengi wanaoishi bila umeme ikiwa ni pamoja na kukidhi mahitaji yake ya kuendesha viwanda.

Muonekano wa mto Rufiji kutokea angani ambao maporomoko yake yatatumika kuzalisha umeme katika mradi unaotarajiwa kujengwa na Serikali wa Stiegler's Gorge.
Sehemu ya mto Rufiji unakatiza katika Pori la Akiba la Selous.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...