THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Tanzania yaeleza ilivyotekeleza mipango ya ICGLR katika kuzuia uvunaji haramu wa madini

Na Teresia Mhagama, Arusha

Katika mkutano wa Kimataifa wa Kamati ya Kikanda inayohusika na upigaji vita uvunaji haramu wa madini katika Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika jijini Arusha 25-27, Julai, 2017, Tanzania ikiwa ni nchi Mwanachama, ilieleza jinsi ilivyotekeleza malengo Sita ya Kamati hiyo ambayo yanapaswa kutekelezwa na nchi wanachama 12 ili kufanikisha udhibiti wa uvunaji haramu wa madini.

Awali, Kamishna Msaidizi wa Madini, Mhandisi John Nayopa alieleza kuwa malengo ya ICGLR ni pamoja na kuwianisha sheria za nchi wanachama ili kuweka uwiano katika sheria za kudhibiti uvunaji haramu wa madini, kuwa na hati moja ya usafirishaji madini ya Tin, Tantalum, Tungsten na dhahabu (3TG) ili kuhakikisha kuwa madini hayo yanachimbwa na kutumika kihalali na lengo la Tatu ni kurasimisha shughuli za wachimbaji wadogo.

Alisema kuwa malengo mengine ya ICGLR ni pamoja na kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za uchimbaji madini, kuimarisha uwazi na uwajibikaji na kuwa na mfumo wa kanzidata utakaowezesha kufuatilia taarifa za uvunaji, usafirishaji na uuzaji wa madini.

Kuhusu uchimbaji wa madini ya 3TG, alisema kuwa, Serikali imeendelea kutoa leseni za uchimbaji wa madini hayo ambapo mpaka sasa zimetolewa leseni 236 za uchimbaji wa madini ya Bati (Tin), leseni 18 za uchimbaji wa madini ya Tantalite, leseni 2 za madini ya wolframite na leseni 11,826 kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ambapo asilimia 95 ya leseni hizo zimetolewa kwa wachimbaji wadogo.

Kuhusu suala la kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji, Mhandisi Nayopa alieleza kuwa Tanzania imeshajiunga na Mpango wa Kimataifa wa Uwazi na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uziduaji (EITI) mwaka 2009 na kuthibitishwa mwaka 2012 ambapo mpaka sasa imeshatoa Ripoti Saba zinazoonesha mapato yanayoingia serikalini kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini, gesi asilia na mafuta na sasa inafanyia kazi ripoti ya mwaka wa Fedha wa 2015/2016 ambapo wananchi sasa wanapata fursa ya kufahamu mapato yanayotokana na uwepo wa Rasilimali hizo.

Kuhusu lengo la ICGLR la kurasimisha shughuli za uchimbaji mdogo wa madini na kuongeza ushiriki wa wanawake katika Sekta ya Madini, Mhandisi Nayopa alisema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kuwa suala hilo linatekelezwa kwa ufanisi ambapo mpaka kufikia mwezi Mei, 2017, takriban leseni za madini 35,000 zimetolewa kwa wachimbaji wadogo huku ikiendelea kutenga maeneo ya uchimbaji madini na kuhimiza uundwaji wa vyama vya ushirika vya wachimbaji wadogo.

Aliongeza kuwa takwimu zinaonesha kuwa kuna makundi na vyama vya wachimbaji wadogo 143 vinavyomiliki leseni za madini ambapo makundi 6 kati ya hayo ni wachimbaji wanawake.

Kuhusu lengo la kuingiza taarifa za madini katika mfumo wa kieletroniki wa kanzidata, Mhandisi Nayopa alisema kuwa Tanzania inao mfumo wa utoaji leseni (Mining Cadastre database) ambao una taarifa za kijiolojia na takwimu mbalimbali za madini na sasa Serikali iko katika hatua za kuboresha mfumo huo ili uendane na mahitaji ya ICGLR.

Kuhusu suala la kuwianisha sheria za madini kwa nchi wanachama wa ICGLR na kutumia hati moja ya usafirishaji madini, Mhandisi Nayopa alieleza kuwa, rasimu za marekebisho katika Sheria ya Madini na kanuni zake zimeashaandaliwa ili kuendana na muongozo wa ICGLR kuhusu Rasilimali zilizopo katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu .

Kuhusu suala la kuwa na hati ya pamoja ya usafirishaji wa madini ya 3TG ifikapo mwaka 2018, Mhandisi Nayopa alieleza kuwa, sambamba na mabadiliko ya hivi karibuni katika sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo yamelenga kuboresha usimamizi katika Sekta ya Madini hali itakayopeleka mabadiliko katika masuala ya utawala kwenye Sekta ya Madini, bado jitihada zinafanyika ili kutimiza lengo la ICGLR la kuwa na hati hiyo ya pamoja.

Akizungumzia Mkutano huo kwa ujumla, Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka alisema kuwa mkutano huo umejikita katika kujadili madini ya 3TG ambayo yanapatikana Tanzania na katika nchi wanachama ili madini hayo yachimbwe kwa mujibu wa taratibu, kuuzwa katika mkondo halali na kuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa jinsi madini hayo yanavyochimbwa mpaka yanapofika kwa mlaji wa mwisho.

Vilevile alisema kuwa mkutano huo pia umejadili suala la ajira kwa watoto katika shughuli za uchimbaji madini ambapo alisema kuwa kwa upande wa Tanzania suala hilo lipo katika sheria ya madini ya mwaka 2010 ambayo sasa imefanyiwa marekebisho ambayo inakataza mtu aliye chini ya miaka 18 kuhusika katika shughuli za madini.
Baadhi ya Wajumbe kutoka Tanzania, Sudan, Sudan Kusini na Rwanda waliohudhuria Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika unaofanyika jijini Arusha. Wa kwanza kushoto ni Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka na wa pili kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Mhandisi John Nayopa.