ERIKALI ya Tanzania, imeshukuru Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) kwa kuwezesha watanzania kupambana na umaskini kupitia miradi wanayoidhamini au kuitafutia fedha. Kwa miongo miwili UNCDF imekuwa ikifanya kazi kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia ofisi ya rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) katika mpango wa kupeleka madaraka kwa umma na shughuli za maendeleo ya kiuchumi . 

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe katika hotuba yake iliyosomwa na Katibu Tawala wa mkoa wa Kilimanjaro Aisha Amour kwenye ufunguzi wa kongamano la siku 2 la Wadau wa Ufugaji Samaki Kibiashara Bwawa la Kalemawe lililoko wilaya ya Same mwishoni mwa wiki.

“Tunafurahishwa kwa namna ya pekee na UNCDF kwa jitihada zake zinazoendeshwa kupitia katika Mpango wa Ufadhili Miradi ya kiuchumi (LFI),” alisema Iyombe na kuongeza: “Tunapokutana hapa tunapewa fursa na kufunuliwa uzoefu wa ushiriki wa UNCDF katika miradi mbalimbali, safari hii tukishuhudia hatua yake ya kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Same katika Mkoa wa Kilimanjaro.” Meneja wa Shamba la Samaki la Ruvu, Khambo Kanthenga (kulia) akitoa maelezo kuhusu mradi wa ufugaji samaki katika shamba hilo kwa viongozi mbalimbali wa Serikali wa wilaya ya Same na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) waliofanya ziara fupi ya mafunzo juu ya ufugaji wa samaki kibiashara katika shamba hilo lililopo wilaya ya Bagamoyo. Kushoto ni mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Mh. Naghenjwa Kaboyoka na Watatu kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Same, Rosemary Staki pamoja na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Mitaji ya Maendeleo (UNCDF)-Tanzania, Peter Malika (wa pili kulia).

 Pamoja na kushukuru kwa hatua mbalimbali zilizofikiwa na taasisi hiyo katika kusaidia watanzania, aliwataka wakazi wa Same kuhakikisha kwamba mradi huo ulioundiwa kampuni ili kwenda kibiashara unafanikiwa na kuwa mfano kwa wengine. Halmashauri ya wilaya ya Same, na jamii inayozunguka bwawa la Kalemawe wanashirikiana na UNCDF kuboresha miundo mbinu ya bwawa hilo na kuwezesha uwapo wa uwekezaji kwa kuanzisha kampuni. 

Kampuni hiyo iliyosajiliwa ya Kalemawe Dam Investment Limited katika mpango maalum (SPV) inamilikiwa na wadau mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya wilaya ya Same, halmashauri ya vijiji sita, wakala wa serikali, watu binafsi pamoja na makundi ya kijamii. Kuwapo kwa kampuni hiyo ni juhudi zinazofanywa za kuwezesha uhusiano mahsusi wa kibiashara unaohusisha ubia wa Serikali, Binafsi na jamii (PPCP) kwa kutoa umiliki linganifu mpaka katika ngazi za chini za mamlaka za kijiji, ambazo kimsingi ndizo wamiliki wa maliasili muhimu ya ardhi kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Vijiji ya Mwaka 1999. Viongozi mbalimbali wa Serikali wa wilaya ya Same na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) wakiwa kwenye ziara fupi ya mafunzo kuhusu ufugaji wa samaki kibiashara katika shamba la ufugaji samaki la Ruvu lililopo wilaya ya Bagamoyo.

Mradi huo wa Ufugaji wa Samaki Kibiashara wa Bwawa la Kalemawe ni zao la ushirikiano kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Same, Kata za Ndungu na Kalemawe, asasi zisizo za kiserikali na wadau wa maendeleo walioazimia kukarabati na kufufua bwawa hilo na mfumo wake wa kilimo cha umwagiliaji. UNCDF kwa kushirikiana na wabia wake waitwao Mikono Tayari (ambao ni kundi linaloundwa na washirika kutoka Tanzania na Norway) ni wataalamu katika mradi hu wa ufugaji samaki kwa pamoja na SPV ya Same na washirika wake. 

Katika kongamano hilo Mkuu wa wilaya ya Same Rosemary Staki amesema wilaya yake ipo tayari kutekeleza mradi huo ambao una manufaa makubwa si tu kwa watu wa Kalemawe na vijiji vinavyozunguka bali pia na halmashauri ya wilaya ya Same. Meneja wa Shamba la Samaki la Ruvu, Khambo Kanthenga (kulia) akitoa maelezo kuhusu vyakula vinavyotumika kulisha samaki wanaofugwa kwenye shamba hilo kwa viongozi mbalimbali wa Serikali wa wilaya ya Same na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) waliofanya ziara fupi ya mafunzo juu ya ufugaji wa samaki kibiashara katika shamba hilo lililopo wilaya ya Bagamoyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...