Mashindano ya mpira wa Miguu maarufu kama URIO CUP 2017 yamezinduliwa rasmi Jijini Dar es Salaam. Mashindano hayo, yanayoratibiwa na Msonge Africa Kwa kushirikiana na Jomo International na kudhaminiwa na Times FM, yana lengo la kuzikutanisha timu 32 zinazotokea katika sehemu mbalimbali za Mkoa wa Dar es Salaam ili kuleta hamasa katika kata ya Kunduchi na pia kuzipa timu za kata hiyo uzoefu. 

Akizindua mashindano hayo, Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio ambaye ndio mdhamini na mwanzilishi wa kombe hilo la Urio Cup alisema hii ni mara ya pili kwa mashindano hayo kufanyika kwani mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2015 na kuhusisha timu 16 na kuongeza kuwa Urio Cup mwaka huu inaenda sambamba na Kampeni maalumu ya ‘Wezesha Mama na mtoto Mpya wa Kuncuchi’ ambayo ilizinduliwa hivi karibuni na yenye lengo la kuboresha zahanati ya Ununio na Mtongani.  Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio akipiga danadana ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Urio Cup mashindano ambayo yanatarajiwa kufanyika katika kata yake kuanzia mwezi ujao. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Radio Times FM, Rehure Nyaulawa, Mratibu wa Urio Cup, Deus Buhilo na Katibu wa Ligi na Mashindano wa Chama Cha Mpira Wilaya ya Kinondoni, Khalid Shehani.

“Moja ya ahadi nilizotoa kwa wananchi wangu ni kuimarisha sanaa na michezo kwani michezo sasa hivi ni chanzo kikubwa cha ajira hasa kwa vijana. Urio Cup iliyopita ilitoa baadhi ya wachezaji waliojiunga na timu za daraja la kwanza na nimefahamishwa kuwa kuna wengine pia wanacheza ligi kuu,” alisema Mh. Urio.

 Alitoa wito kwa wadau mbalimbali wapenda michezo wamuunge mkono katika hili ili kombe hili liweze kukua mwaka hadi mwaka na kuwafadisha vijana wengi zaidi. “Nimearifiwa kuwa tutawaalika wawakilishi kutoka timu za ligi kuu ili waweze kutafuta vipaji kutoka kwa timu zitakazoshiriki Urio Cup. 

Hili litasaidia sana katika kuamsha ari ya vijana huku wote wakiwa na matumaini ya kusajiliwa na timu kubwa siku moja,” alisema diwani huyo. Naye mratibu wa Urio Cup, Bw. Deus Buhilo alisema maandalizi yote yamekamilika na wanatarajia kushindanisha timu 32 ambazo zinatakiwa kujisajili na kulipia ada ya Tsh 70,000 na timu zinazotakiwa kujisajili zinatakiwa kutuma maombi na kupata maelekezo kupitia namba 0652559122 na malipo kupitia namba 0628555333. 
 Diwani wa Kata ya Kunduchi, Michael Urio akizungumza wakati wa uzinduzi wa Urio Cup mashindano ambayo yanatarajiwa kufanyika katika kata yake kuanzia mwezi ujao. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Radio Times FM, Rehure Nyaulawa na Katibu wa Ligi na Mashindano wa Chama Cha Mpira Wilaya ya Kinondoni, Khalid Shehani.

“Urio Cup ni mashindano makubwa na tumeweka vigezo ili kuhakikisha tunakuwa na mashindano bora yanayofuata kanuni zote za FIFA na TFF. Tunataka kuwajengea vijana wetu uzoefu ili waweze kufika katika ngazi za juu zaidi,” alisema mratibu huyo na kumshukuru Diwani Urio kwa kuanzisha mashindano hayo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...