THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

WAAJIRI NCHINI WATAKIWA KUZINGATIA MGAWANYO SAHIHI WA RASILIMALIWATU

Waajiri nchini wametakiwa kuzingatia mgawanyo sahihi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ili kuwa na utendaji bora na wenye matokeo katika utumishi wa umma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Mhe. Kairuki amesema mwajiri anapoomba kibali cha kuajiri watumishi ni vema akazingatia mahitaji kulingana na majukumu yaliyopo ili kuondoa ziada ya watumishi wa umma wasio na kazi kuendana na fani walizosomea kwa lengo la kuwa na utendaji mzuri.

“Ni vizuri sana wakati tunaomba vibali vya kuajiri watumishi wa umma tukazingatia mgawanyo sahihi wa rasilimaliwatu katika maeneo yetu kulingana na majukumu ya watumishi tunaowahitaji badala ya kuomba watumishi wengi ambao wanasababisha kuwa na ziada ambayo haitumika ipasavyo” Mhe. Kairuki amesema.

Waziri Kairuki amesema katika vibali 10,184 vilivyotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti za Mikoa, Wakala za Serikali, pamoja na Taasisi na Mashirika ya Umma ili kujaza nafasi zilizoachwa na watumishi wa umma waliobainika kughushi vyeti vya elimu, Halmashauri ya Manisapaa ya Ubungo imetengewa jumla ya nafasi 140.

Aidha, ameongeza kuwa, Halmashauri hiyo imetengewa jumla ya nafasi za ajira mpya 397 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hivyo zitendewe haki kwa kuhakikisha watumishi watakaoajiriwa wanafanya kazi kwa mujibu wa mpango uliopo.

Mhe. Kairuki yuko katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es salaama kwa lengo la kukutana na watumishi wa umma na kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini ili kufikia malengo yaliyopangwa na Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Kisare Makori akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) katika Ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam leo.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Kisare Makori akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) kuzungumza katika kikao kazi na viongozi na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi katika Manispaa hiyo leo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akizungumza na viongozi na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo (hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi katika Manispaa hiyo ili kupokea maoni, ushauri na kusikiliza kero za watumishi wa umma leo Jijini Dar es Salaam.