Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim (katikati) akielezea mikakati ya jumuiya hiyo ya kuwezesha wadau mbalimbali wataoshiriki katika utoaji wa huduma kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 02 Agosti, 2017. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim, amesema kuwa jumuiya inakaribisha makampuni mbalimbali nchini kujiunga na jumuiya hiyo na kuwezeshwa kwenye ushiriki katika mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Abdulrahim aliyasema hayo leo kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam na kushirikisha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, na watendaji kutoka Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na  Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF).

Alisema kuwa tayari baadhi ya makampuni yameshaanza kujiunga na jumuiya hiyo na kutaka watu binafsi wenye nia ya kushiriki katika utoaji huduma kwenye mradi wa bomba la mafuta kujiunga na jumuiya hiyo ili kuwezeshwa. Alisema kuwa kazi kubwa itakayofanywa na ATOGS ni pamoja na kuwawezesha washiriki kupata utaalam wa utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja na namna ya kupata mikopo kwenye mabenki na taasisi mbalimbali za kifedha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye (katikati) akifafanua jambo katika mkutano huo. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim.

Aidha, alipongeza jitihada za serikali katika kuwezesha uchumi wa viwanda kupitia mradi wa bomba la mafuta hali inayoleta matumaini ya kuwa nchi kutoka kwenye orodha ya nchi masikini duniani na kuingia katika orodha ya nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 kama Dira ya Maendeleo ya Taifa, inavyofafanua.

 Alisisitiza kuwa lengo la jumuiya ni kuwaunganisha watoa huduma wote na kuwapa elimu ya namna bora ya utoaji wa huduma ili kuweza kushiriki kikamilifu katika mradi wa bomba la mafuta. Aliongeza kuwa mradi wa bomba la mafuta utaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kuanzia kwa mwananchi mmoja mmoja hadi kwa taifa kwa ujumla na kuwataka wananchi hasa waishio katika mikoa itakayopitiwa na miundombinu ya bomba la mafuta kuchangamkia fursa na kuondokana na umasikini.

Aliendelea kutaja mikoa itakayopitiwa na miundombinu ya bomba la mafuta kuwa ni pamoja na Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara na Tanga. Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo alipongeza uanzishwaji wa ATOGS na kusema kuwa jumuiya hiyo imekuja wakati mwafaka wa mradi wa bomba la mafuta na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa zilizopo kupitia jumuiya hiyo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa pili kushoto) akifafanua jambo katika mkutano huo. 

Dkt. Pallangyo alitumia fursa hiyo kuwakaribusha watanzania kujitokeza katika uzinduzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania unaotarajiwa kufanywa na Marais Yoweri Museven wa Uganda na Dkt. John Magufuli siku ya Jumamosi wiki hii. Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF).

Godfrey Simbeye aliyataka makampuni yatakayopata tenda ya kutoa huduma kwenye mradi wa bomba la mafuta kufanya kazi kwa umahiri na uadilifu mkubwa kwa manufaa ya nchi.

“ Kutakuwepo na kazi nyingi sana zitakazotolewa kwa watanzania hususan huduma kwa wakandarasi watakaojenga bomba, umakini na uadilifu wa hali ya juu unahitajika ili kuleta sifa njema kwa nchi,” alisema Simbeye Aliishauri serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuweka mpango maaalum wa kutoa mafunzo wa namna ya kujenga mabomba ili baadaye wataalam wa ndani ya nchi wafanye kazi ya kujenga mabomba na kupunguza gharama.

Aliendelea kusema kuwa wakati serikali ikiimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, mabenki yajiandae kutoa mikopo mara moja kwa makampuni yatakayopata tenda kwenye mradi wa bomba la mafuta.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...