Sehemu ya walengwa wa kaya maskini wakiwa katika zoezi la kupokea ruzuku kijij cha Mwigumbi.

Na Robert Hokororo.

Kaya  6019 katika halmashauri ya wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, zinatarajia kunufaika na fedha sh. milioni 204.6 zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu. Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF wilayani humo, Sospeter Nyamuhanga ofisini kwake wakati akizungumzia zoezi la uhawilishaji fedha hizo linalotarajiwa kuvifikia jumla ya vijiji 78.

Alisema kuwa zoezi hilo linatarajiwa kuanza kufanyika kuanzia Agosti 7 hadi 11 mwaka huo katika vijiji lengwa kwenye kata zilizo katika mpango wa TASAF III wilayani humo .
Nyamuhanga alifafanua kwa kusema kuwa zoezi la uhawilishaji fedha kwa kaya hizo linaanza kwa lengo la kuziwezesha kaya maskini ili zikwamuke kutoka hali ya umaskini.

Mratibu huyo alisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2016/2017 jumla ya wanakaya 54 wameingizwa kwenye mpango huo wa TASAF III wakiwemo watoto waliozaliwa katika kipindi hicho.

“Lengo la mpango wa TASAF ni kuhakikisha walengwa wanatimiza masharti kama ya kuwapeleka watoto shule ili baadaye wapate elimu ambayo itawaondoa katika umaskini na pia kuhakikisha wanawapeleka kwenye huduma za afya kupitia fedha hizi,” alisema. Mratibu huyo aliongeza kwa kubainisha kuwa mpango wa TASAF wilayani Kishapu umeonesha mafanikio yakiwemo baadhi ya kaya kubadilika kimaisha kwa kufuga mifugo kama ng’ombe na mbuzi.

Alisema kuwa baadhi ya walengwa tayari wamebadilisha aina za makazi yao kutoka nyumba za tembe na nyasi na kuanza kujenga nyumba za kisasa za bati hali inayoleta matumaini katika miradi kama hii.
Mratibu huyo amesema mfuko huo unatoa ruzuku za aina mbili, ya msingi inayotolewa kwa kaya zote masikini zilizoandikishwa kwenye mpango na nyingine ni ya utimizaji masharti ambayo hutolewa kwa kaya zenye watoto wanaotakiwa kwenda shule na vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha,  Nyamuhanga aliwataka wanufaika kuwa na matumizi sahihi ya fedha wanazopata ili lengo la TASAF la kuwatoa katika umaskini na kuwafanya wajitegemee litime.

Kishapu ni miongoni mwa halmashauri za wilaya 161 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba zinazotekeleza Mpango wa TASAF III ili kuongeza kipato na fursa za kuboresha upatikanaji wa mahitaji muhimu.
Walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini unaoendeshwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani Kishapu wakiwa katika zoezi la kupokea ruzuku katika kijiji cha Mwigumbi kata ya Mondo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...