Kumekuwa na mjadala wa muda mrefu kuhusu TEF. Licha ya kasoro zake, pengine TEF kwa sasa ndiyo jumuiya ya waandishi wa habari Tanzania yenye umaarufu zaidi kuliko zote. Moja ya tuhuma kubwa dhidi ya TEF ni kuwa jukwaa hili limekuwa linatumika kama "kichaka" ambacho viongozi wa taasisi mbalimbali (hususan za umma) hujificha ili kujikinga na tuhuma za ufisadi.
TEF pia imekuwa inajulikana kwa kutoa matamko ya kufungia au kufungulia watu fulani wasiandikwe na vyombo vya habari nchini. Suala ambalo sisi wengine ambao siyo wanachama wa TEF tumekuwa tunahoji ni kuwa TEF ni jukwaa la wanachama (members only), hivyo basi, wanachama wa TEF wana *haki* ya kualikwa kwenye mikutano ya TEF na semina zinazoandaliwa na TEF na wana *wajibu* wa kupokea na kutekeleza maagizo ya TEF. Kwa muktadha huo huo, wahariri na waandishi ambao sio wanachama wa TEF hawana haki ya kuitwa kwenye vikao vya TEF, na hawana wajibu wa kutekeleza maagizo ya TEF.
Kumekuwa na dhana potofu kuwa maagizo na maamuzi yote ya TEF ni lazima yatekelezwe na waandishi wote wa habari, wahariri na taasisi zote za habari za Tanzania, hata wale wasio wanachama wa TEF bila kuzingatia dhana ya haki na wajibu.
Mara kadhaa tumesikia wahariri au vyombo vya habari vikiitwa wasaliti kwa kutotekeleza maagizo ya TEF bila kujali kama wahariri hao ni wanachama wa TEF au la. Je, ni nani amewapa TEF mamlaka ya kuwa wafanya maamuzi, watoa amri na wasemaji wa waandishi wa habari, wahariri na vyombo vyote vya habari vya Tanzania?

Lazima ieleweke wazi kuwa wenye wajibu wa kutekeleza maamuzi ya TEF ni wahariri ambao ni wanachama wa TEF tu. Wahariri ambao sio wanachama wa TEF hawana wajibu wowote ule wa kupokea maagizo ya TEF. Ni jukumu la TEF kuwashawishi wahariri hao waungane na msimamo wao kwa kujenga hoja.
Ni vyema TEF ikajitathmini na kurekebisha hii taswira mbaya iliyopo. Je, kuandaa semina ambazo wahariri wanalipwa posho na kufungia/kufungulia watu fulani wasiandikwe na vyombo vya habari ndiyo jukumu kubwa la TEF?
Ningependa kuona TEF ikijikita kukabiliana na matatizo ya msingi zaidi yafuatayo kwenye tasnia ya habari ya Tanzania:

1. Tatizo la rushwa kwenye tasnia ya habari ya Tanzania

2. Kuhakikisha kuwa baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari Tanzania wanaacha kutoa maslahi duni kwa waandishi wa habari na kuhakikisha waandishi wa habari wanakuwa katika mazingira mazuri ya kazi

3. Kuondoa tatizo sugu la kuporomoka kwa maadili na weledi kwenye tasnia ya habari ya Tanzania

4. Kukemea na kukabiliana na kuongezeka kwa vitendo vya kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Tanzania

5. Kutoa dira kuhusu hatma ya vyombo vya habari nchini Tanzania kutokana na mazingira magumu ya biashara hiyo nchini kwa sasa

Pale ambapo TEF itakapojitathmini, naamini kwa dhati kuwa ina fursa kubwa ya kuwa jukwaa lenye nguvu na linaloheshimiwa na kuungwa mkono na waandishi wa habari na wananchi wengi zaidi nchini.

Naomba kuwasilisha.
Fumbuka Ng'wanakilala, 15 Agosti 2017

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...