Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha

WAZIRI wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Nchemba, amewataka askari wa uhamiaji nchini kuhakikisha wanataifisha magari na vyombo vya usafiri wanavyokutwa navyo wahamiaji haramu, wakati wanapokamatwa. Aidha amewaagiza askari hao kuwakamata watu wanaowalipia faini wahamiaji haramu na kuwafungulia mashitaka.

Mwigulu aliyasema hayo, wakati alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi za mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA) na ofisi mpya ya uhamiaji ya mkoa wa Pwani ambazo zote zipo wilayani Kibaha. Alisema magari na vyombo vinavyosafirishia wahamiaji haramu ikiwemo boti vitaifishwe na kutumika katika kazi za ujenzi wa taifa.


"Haiwezekani mtu aingie nchini kwa makusudi bila kibali halafu inapotakiwa kulipa faini kutokana na kosa hilo atokee mtu kuwalipia faini kwa haraka jambo linalosababisha vitendo hivyo kuenea kwa kasi” alisema Mwigulu.

Mwigulu alieleza kwamba, ni lazima iangaliwe, jamii inapaswa kujiepusha na kushirikiana na kundi hilo ili kupunguza wimbi kubwa la wahamiaji haramu nchini. Waziri huyo alisema, iangaliwe njia  za kudhibiti wahamiaji hao pale inapotokea kukamatwa ama kushtakiwa  na kuhukumiwa pasipo kuwalinda kwa kuwalipia faini.

"Mkiwakamata pia na magari myataifishe siku hiyo hiyo na kuyapeleka magereza ili yakabebe mawe, na hata mkiwakamata kwenye boti taifisheni hizo boti hakuna kuweka viporo"alisema Mwigulu.

Awali akitembelea ofisi mpya katika jengo la vitambulisho vya taifa (NIDA), Mwigulu aliwaagiza watendaji wa ofisi hiyo kuhakikisha wanafanyia kazi agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuunganisha utambulisho wa jumla kwa wananchi.

"Wananchi wanatakiwa wawe na utambulisho wa aina moja pekee unaojumuisha taarifa zao zote" alisisitiza Mwigulu.

Nae afisa Uhamiaji Mkoani Pwani, Plasida Mazengo alisema ofisi yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa vitendea kazi hali inayosababisha kufanyakazi kwenye mazingira magumu. Alimuomba waziri huyo kuangalia namna ya kusaidia kutatua changamoto hizo ili waweze kufanya kazi zao kifanisi zaidi kwa maslahi ya watanzania.

Kaimu mkurugenzi wa uzalishaji vitambulisho (NIDA) Alfonce Malibiche alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo umefikia asilimia 99.9, na utakapokamilika utawarahisishia wananchi kupata huduma kirahisi na jengo litaanza kazi rasmi mwishoni mwa mwezi huu .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...