Na: Judith Mhina – MAELEZO

Hakika historia imejirudia, mkoa wa Tanga ni kati ya mikoa mashuhuri nchini Tanzania kabla ya uhuru wa Tanganyika katika kupigania uhuru, kwa kuwa ni mkoa uliokuwa na wasomi wengi kuliko mikoa mingine wakati huo.

Hii ilitokana na uwepo wa shule za wamisionari wa kanisa la Anglikana (UMCA) ambalo ni la kwanza kuingia katika Pwani ya Afrika Mashariki mwaka 1878 na waliojenga shule za Magila na Kiwanda Muheza, Korogwe misheni, Kideleko Handeni (Shule za Kati) na Saint Andrew Minaki Pwani (shule ya Sekondari).

Hata baada ya uhuru chini ya Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere na Rais Msataafu Ali Hassan Mwinyi, mkoa wa Tanga ulikuwa maarufu kutokana na uwepo wa viwanda vingi, njia za reli na Bandari yenye kina kirefu yenye uwezo wa kuingiza meli kubwa za mizigo za Kitaifa na Kimataifa.

Viwanda ambavyo vilijengwa katika mkoa wa Tanga ni pamoja na vya chuma, mbolea, saruji, maziwa, kamba za katani na mazulia, amboni plastic, mbao, sabuni maarufu ya mbuni, gardenia, foma na mafuta ya nazi.

Historia hii sasa inajirudia katika mkoa wa Tanga baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli, kupigania kwa nguvu zote Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuja nchini Tanzania ambalo litaishia katika kijiji cha Chongoleani.

Wananchi wote wa Tanzania wana kila sababu ya kujivunia ujenzi wa bomba hilo la mafuta ambalo litawapatia ajira Watanzania hususan wananchi wa mkoa wa Tanga. Pongezi kubwa ziende kwa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za kuhakikisha kwamba Mradi huu unakuja Tanzania. Wananchi wa mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kulinda heshima ya nchi yetu kwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ulinzi mkali wa Bomba hilo kila mahali lilikopita.

Kurejea kwa mkoa wa tanga katika ramani ya Tanzania ya viwanda umedhihirishwa na Wananchi wa Chongoleani ambao siku ya uwekaji jiwe la msingi walikuwa wawakilishi wa Watanzania ambao hawakupata fursa ya kwenda Tanga kumshuhudia Mheshimiwa Rais na na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni wakifungua pazia la jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa Mradi huo.

Kutokana na tukio hilo la uwekaji wa jiwe la msingi wana Chongoleani walitoa ya moyoni kwa kuonyesha furaha yao isiyo na kifani kupitia kwa Mwenyekiti wao wa kijiji Ndugu Mbwana Nondo wakisema; “Kwa moyo wa dhati kabisa tunamshukuru sana Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutujali Wananchi wake kwa kutuletea neema ya mradi huu wa bomba la mafuta”.

Aidha, Mwenyekiti huyo aliongeza kwa kusema kwamba, katika maisha yetu Wananchi wa Chongoleani hatutaweza kumsahau Mheshimiwa Rais kwa mambo mengi anayowafanyia Watanzania na Taifa kwa ujumla na itakuwa ni kumbukumbu kwa kizazi kijacho.

“Napenda kusisitiza kwamba tunamuahidi Rais, kuwa wote watakaopata fursa kwenye Mradi huu wa Bomba la Mafuta, watafanyakazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla”. Alihitimisha Bw Nondo.

Naye Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Bibi Ummy Mwalimu, amewaomba wanawake wa Mkoa wa Tanga kuchangamkia fursa zinazojitokeza, kutokana na uwepo wa mradi wa bomba la mafuta.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...