THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

NEC YAPONGEZWA KWA USIMAMIZI NA MATUMIZI BORA YA RASILIMALI ZA SERIKALI

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani (Kulia) akimweleza jambo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) alipotembelea Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi eneo la kuhifadhia Mashine za BVR. Katikati ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge), Maimuna Tarishi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuendelea kusimamia matumizi bora ya rasilimali inazopewa na Serikali na kuzitaka taasisi nyingine za Serikali kuiga mfano huo.

Mhe. Muhagama ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam mara baada ya kutembelea ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuangalia utekelezaji wa maagizo ya Bunge kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Bora iliyoridhia Bunge lipitishe fedha kiasi cha shilingi bilioni 10 kuiwezesha Tume kufanya maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini .

Akizungumza na watendaji na baadhi ya watumishi wa Tume amesema kuwa ameridhishwa na utendaji kazi wao na namna Tume ilivyojipanga kutekeleza jukumu la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuelekea uchaguzi ujao wa mwaka 2020 kwa kuwa na mpango Kazi, unaochambua na kubainisha mahitaji muhimu yanayotakiwa, lini na wapi ili kazi hiyo iweze kufanyika kwa umakini. 
 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akitazama moja ya Daftari la Wapiga Kura alipotembelea Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi jijini Dar es salaam. Katikati ni Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani na Kushoto ni Afisa TEHAMA wa Tume Bi. Mwamvita Solo.

“ Naipongeza sana Tume kwa kuendelea kufanya vizuri , nimegundua kuwa imejipanga vizuri kutekeleza majukumu yake ambayo yameainishwa Katika Katiba,  kwa niaba ya Waziri Mkuu nimekuja hapa na timu ya watendaji kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kuangalia utekelezaji wa maagizo ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala Bora walioridhia Bunge lipitishe fedha shilingi Bilioni 10 ili kuiwezesha kufanya maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura” Amesema.

Mhe. Mhagama ameeleza  kuwa kazi hiyo kazi ya utekelezaji wa maagizo hayo ya Bunge inazingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 5 kifungu kidogo cha 3 (a) ambacho kimeweka uanzishwaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura nchini na Ibara ya 74 kifungu kidogo cha 6 (a) na (e) ambacho kinaipa Tume madaraka ya kuchukua jukumu la kuandikisha wapiga Kura nchini Tanzania.
Afisa TEHAMA wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Julius Kobelsiki akitoa ufafanuzi kuhusu Mashine ya kuandikisha Wapiga Kura ya BVR kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea Ofisi za Tume jijini Dar es salaam.

Aidha, ameongeza kuwa Sheria ya Uchaguzi kifungu cha 15 (3) kinaipa madaraka Tume ya Uchaguzi  kutengeneza mfumo na utaratibu wa  uandikishaji wa wapiga Kura nchini na uboreshaji wa daftari hilo mara mbili kati ya Uchaguzi mkuu mmoja na unaofuata.

“Tunaelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa hiyo ili tuzingatie takwa la Katiba na takwa la Sheria ya Uchaguzi ambayo inasimamiwa na Tume ni lazima sasa Serikali ione kwamba inaisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wote tunajua kuwa utendaji wake ni huru lakini Serikali tunaowajibu wa kuhakikisha kuwa Tume inafanya kazi yake vizuri” Amesisitiza.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge), Maimuna Tarishi akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ziara hiyo ameipongeza uongozi wa Tume  kwa kuonyesha mfano katika kuondoa mazoea katika utendaji kazi ikiwemo utunzaji wa mali na rasilimali za Serikali.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira na Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na baadhi ya watendaji na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika Ofisi za Tume jijini Dar es salaam. Kulia kwake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Waziri Mkuu na Bunge), Maimuna Tarishi na Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani (kulia). Picha na Aron Msigwa.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuijengea uwezo Tume kwa kuipatia rasilimali na vitendea kazi inavyohitaji ili iweze kutimiza majukumu yake kwa wakati.

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani akizungumza mara baada ya kumalizika kwa ziara hiyo amemshukuru viongozi hao kwa kuzitembelea ofisi za Tume kuangalia maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuishukuru Serikali kwa kutenga shilingi Bilioni 10 zitakazotumika kwa ajili ya uboreshaji huo.

 Amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi imejipanga kulitekeleza jukumu hilo kikamilifu na inaendelea kufanya maandalizi mbalimbali yakiwemo ya kuzipitia Mashine za BVR zitakazotumika kuandikisha wapiga Kura , kupitia mifumo Sheria na kanuni za Uboreshaji, kupitia vifaa vilivyopo ili kupunguza mzigo wa kununua vifaa vipya wakati wa zoezi hilo.