Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam

Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa Kanuni za taarifa za Usafirishaji na uingizaji wa fedha taslimu kutoka na kwenda nje ya nchi (Crossborder Declaration of Currency and Bearer Negotiable Instruments Regulations) ambapo wasafirishaji wa fedha taslimu na wasafiri wote wanaotoka au kuingia nchini, watatakiwa kutoa taarifa za fedha taslimu wanazosafirisha ikiwa fedha hizo zinalingana au zinazidi kiasi cha dola za kimarekani elfu kumi (USD 10,000).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni hizo, Kamishna na Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) Ndugu Onesmo H. Makombe alisema utekelezaji wa kanuni hizi, pamoja na mambo mengine utaiwezesha nchi kuwa na takwimu za usafirishaji fedha taslimu.

“Takwimu hizo zitakazosaidia pamoja na mambo mengine kubaini vitendo vya kihalifu, kupunguza utoroshaji wa mitaji na kuhakikisha kuwa tunapunguza kama siyo kumaliza kabisa usafirishaji wa fedha zitokanazo na uhalifu au/na fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi” alisema Bw. Makombe

Aidha kanuni hizo zimeweka adhabu zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakabainika kutaka kupita na fedha zinazolingana au zinazozidi kiwango kilichowekwa bila kutoa taarifa au watakaotoa taarifa za uongo. Alizitaja adhabu hizo kuwa ni pamoja na kukamatwa kwa fedha taslimu walizonazo na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria kama vile kufunguliwa mashtaka.

“Wahalifu pamoja na mambo mengine, wanapenda kusafiri na fedha taslimu kwani wanaogopa kutumia benki kutuma fedha kutokana na umakini unaoongezeka katika benki na udhaifu unaoweza kuwepo mipakani” Alisisitiza Bw. Makombe.Kamishna huyo amewaasa washiriki wa warsha hiyo kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ili kuziba mianya yote ambayo wahalifu wanaweza kuitumia kutimiza kusudi lao ovu na kuhatarisha usalama wa nchi.

Washiriki wa warsha ya siku mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni za Taarifa za Usafirishaji na uingizaji wa fedha tasilimu kutoka na kwenda nje ya nchi wakifuatilia kwa makini mjadala katika warsha hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa warsha ya siku mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni za Taarifa za Usafirishaji na uingizaji wa fedha tasilimu kutoka na kwenda nje ya nchi wakiwa katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa warsha hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), jijini Dar es Salaam.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango).



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...