Makamanda wa vyombo vya ulinzi na usalama mkoani Lindi wamewataka wananchi kutunza vizuri fedha zao ili kupunguza uharibifu unaoliongezea taifa gharama za kutengeneza fedha zingine.

Aidha, viongozi hao wameelezea umuhimu wa wananchi kutambua alama za usalama wa noti zetu ili kuepuka kuangukia mikononi mwa matapeli na kupata hasara.

Viongozi hao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, SACP Renatha Mzinga, Mkuu wa Magereza wa Mkoa, Bw. R. Nyange, na Mkuu wa Usalama wa Taifa wa Mkoa wa Lindi, Bw. Nsiima Wema walisema hayo baada ya kutembelea banda la Benki Kuu ya Tanzania katika maonesho ya Wakulima kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi. 

RPC Mzinga alisema taifa linaingia hasara kubwa kutengeneza noti zinazotokana na uharibifu unaofanywa mara kwa mara na wananchi.

“Mimi nilikuwa najua pesa chafu zinarudishwa Benki Kuu na kufanyiwa recycling na kurudishwa kwenye mzunguko; kumbe tunapata hasara. Kwa elimu hii niliyoipata, nawashauri wananchi kwa ujumla watunze fedha zetu, kwa sababu zinapoharibika ni hasara kwa taifa,”alisema RPC Mzinga.

Mkuu wa Usalama wa Taifa mkoani Lindi, Bw. Wema alieleza kwamba amefurahishwa sana kwa kupata elimu kuhusu alama za usalama za noti zetu na kuahidi kutumia elimu hiyo kuwafundisha wengine.

“Kikubwa zaidi kilichonivutia ni namna ya kutambua pesa halali na pesa zisizo halali. Kwa ajili ya kukosa uelewa wananchi wengi wanalizwa kila siku kwa kupewa pesa zisizo halali kwa kuwa hawajui kuzitambua. Elimu niliyoipata itanisaidia niwaambie na wenzangu mtaani kwamba pesa halali iko hivi na isiyo halali iko hivi,” alisema Bw. Wema.

Mkuu wa Magereza wa Mkoa, Bw. Nyange, aliwashauri wananchi wanapofikia umri wa kustaafu wajiepushe kuwekeza katika biashara wasizozijua ili kuepuka hasara na badala yake wawekeze katika dhamana za serikali zinazotoa faida ya uhakika bila wasiwasi wowote wa kuingia hasara.

“Watu wanapostaafu mara nyingi wanajiingiza kwenye miradi mbalimbali…ambayo hawana ujuzi nayo; hawajui hata hasara zake, ili mradi wanaona mtu fulani ana biashara ya magari, ana mabasi, basi naye anajiingiza huko matokeo yake anapata hasara au mwingine anajiingiza kwenye mashamba na wakati mwingine jua mwaka huo linakuwa kali, moja kwa moja mazao yanakufa, inafikia hatua mtu anaweza hata kujiua…kumbe fedha ile unaweza ukawekeza kwenye dhamana za serikali, ukaendelea kupata faida na pesa yako ikabaki kuwa salama,” alisema.

Viongozi hao wa vikosi vya ulinzi na usalama mkoani Lindi walitumia takriban saa nzima wakipata elimu ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Benki Kuu na jinsi zinavyoendana na Kauli Mbio ya Maonesho ya Wakulima ya mwaka huu isemayo: Zalisha kwa tija mazao na bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi ili kufikia uchumi wa kati.

Maonesho ya Nane Nane kitaifa mwaka huu yalifunguliwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Bw. George Simbachawene tarehe 1 Agosti, 2017, ambaye pamoja na mambo mengine aliwataka wakulima, wafugaji na wavuvi kuongeza tija kwa kuzalisha mazao na bidhaa kwa njia za kisasa.

Waziri Simbachawene alihimiza kilimo na ufugaji wa kisasa na kuwataka wavuvi kuanzisha ufugaji wa kisasa kwa kujenga mabwawa badala ya kutegemea mitego katika mito, maziwa na bahari, ambako hakuna uhakika wowote wa kipato.Maonesho kama haya pia yanafanyika katika ngazi ya kanda katika kanda za Mashariki, Kati, Ziwa, Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...