WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzia sasa ni marufuku kuweka bei ya tumbaku kwa dola za Marekani kwa sababu imechangia kuwaumiza wakulima wa zao hilo. 
 Amesema wanunuzi wa zao hilo wana uhuru wa kuweka bei zao kwa dola lakini bei hiyo itafsiriwe kwa shilingi za Kitanzania ili wakulima waweze kutambua bei elekezi tangu mwanzo wa msimu. Ametoa kauli hiyo Jumatano, Agosti 9, 2017 wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora. 
 Hivi sasa bei elekezi kwa msimu huu wa tumbaku ni dola mbili za Marekani kwa kilo moja ya tumbaku sawa na sh. 4,400 hadi sh. 4,500 za Tanzania. 
 Hata hivyo, Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani hapa, alionya juu ya mkanganyiko unaowapata wakulima na viongozi wa vyama vya msingi (AMCOS) kwenye kutafsiri bei ya zao hilo kutoka dola za Marekani. 
 “Kwa mfano, mkulima anapouza tumbaku anaambiwa kilo zake zina thamani ya dola za marekani 90. Wakati anapokuja kulipwa bei ya shilingi inakuwa imebadilika, kwa hiyo kama aliuziwa wakati thamani ya dola moja ikiwa ni sh. 1,500/- na wakati wa kulipwa imefikia sh. 2,000/- hatalipwa kwa bei ya sasa. Bali atalipwa kwa bei ileile ya zamani jambo ambalo linamuumiza mkulima,” amesema. Akiwa hapohapo ukumbini, Waziri Mkuu aliwauliza wawakilishi wa benki za CRDB na NMB bei ya dola moja ni sawa na shilingi ngapi kwa hapo Tabora, alijibiwa kwamba katika benki ya CRDB, dola moja ya Marekani inauzwa kwa sh. 2,200 ilhali katika benki ya NMB, dola moja inauzwa kwa sh. 2,167.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...