THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

NEWS ALERT: MWANZILISHI WA DOGODOGO CENTRE NA NYUMBA YA SANAA MAREHEMU SISTER JEAN PRUITT KUZIKWA JUMATANO IJAYO JIJINI DAR ES SALAAM

Mazishi ya mwanzilishi wa Kituo cha Kulelea watoto wa mitaani cha Dogodogo Centre na Kituo cha Sanaa na Utamaduni cha Nyumba ya Sanaa Marehemu Sister Jean Pruitt aliyefariki Septemba 10, 2017 huko Karatu mkoani Arusha yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano ijayo jijini Dar es salaam. 
Kwa mujibu mmoja wa vijana waliolelewa naye, Ndugu Amos, mwili wa Sister Jean unatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam siku ya Jumanne ama Jumatano hiyo hiyo wiki ijayo. Taarifa za taratibu na ratiba kamili zitatolewa mara baada ya maandalizi kukamilika. 
Sister Jean Pruitt aliletwa Tanzania mwaka 1969 na na taasisi ya kidini ya Marekani ya Maryknoll Sisters kufanya kazi na Kanisa Katoliki, akianza kushughulika na taasisi ya Misaada ya Catholic Relief Services, akishughulika zaidi na maendeleo ya afya ya vijana na watoto wa Tanzania. 
 Toka awasili nchini miaka hiyo, alianzisha taasisi nyingi zilizosaidia sana wasanii, walemavu na watoto na vijana walio katika mazingira magumu. 
Mwaka 1972 alianzisha kituo cha utamaduni cha Nyumba ya Sanaa jijini Dar es salaam ambacho kikaja kuwa mojawapo ya taasisi mashuhuri alizoanzisha na zilizofanikiwa sana. 
 Uwanja ilipojengwa Nyumba ya Sanaa hivi sasa ni makao makuu ya benki ya NMB, ambao kwa kutambua umuhimu wake, wametenga sehemu moja kwa ajili ya Nyumba ya Sanaa. Lakini sio kubwa kama ilivyokuwa yenyewe kabla ya kuvunjwa, jambo ambalo Sister Jean alililalamikia sana sana, hasa ikizingatiwa yeye binafsi aliomba eneo hilo toka kwa Rais wa wakati huo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, na alipolipata lilisaidia sana kukuza sanaa ua utamaduni wa Mtanzania. 
 Mwaka huo huo wa 1972 alianzisha tawi la Caritas, na mwaka 1988 alikuwa mwanzilishi mwenza wa chama cha Urafiki wa Tanzania na Msumbiji (TAMOFA). 
 Mwaka 1992 Sister Jean alianzisha kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Dogodogo Centre kukabiliana na ongezeko la watoto hao jijini Dar es salaam. Alifanikiwa sana na watoto na vijana na watoto wengi waliolelewa hapo hivi sasa ni watu wazima wakifanya shughuli zao. 
 "Ni majonzi makubwa sana kwangu na jamii ya Tanzania kwa ujumla wake maana mchango wake ni mkubwa mno kwa familia nyingi hapa nchini" anasema Amos ambaye alilelewa hapo Dogodogo Centre toka mwaka 2002 hadi mwaka 2009. Hivi sasa yeye ni producer mashuhuri wa vipindi vya TV.
Marehemu Siter Jean Pruitt
17 October 1939–10 September 2017

Kusoma habari zake zaidi BOFYA HAPA