Timu ya wataalamu kutoka Jukwaa la Haki Jinai iliyoko mkoani RUVUMA imetembelea magereza ya KITAI na MBINGA pamoja na Kituo cha Polisi Wilaya ya MBINGA. 

Timu hiyo ya wataalamu inayoongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome imekutana na kuzungumza na mahabusu na wafungwa walioko katika magereza hayo kuhusiana na changamoto wanazokabiliana nazo wakiwa ndani ili kuweza kupata haki zao kwa wakati.

Timu hiyo imetumia nafasi hiyo kutoa huduma na ushauri kwa wafungwa na mahabusu hao huku ikiwataka kuishi vyema wakiwa katika magereza. Timu hiyo pia imewataka wafungwa na mahabusu hao kuhakikisha wanaishi kwa kutii sheria bila ya shuruti na hivyo kuwa raia wema.

Timu hiyo ilipotoka katika magereza hayo ilitembelea Mahakama ya Wilaya ya Mbinga na kuwasilisha changamoto zinazowakabili wafungwa na mahabusu walioko katika magereza ya Mbinga na Kitai ili kuweza kuhakikisha mahakama hiyo inayafanyia kazi malalamiko ya watuhumiwa hao.

Ziara hiyo ni miongoni mwa ziara ambazo zimeshafanyika katika mikoa ya Iringa na Njombe zilizolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi walioko jela na vizuizini katika harakati za kupata haki zao kwa wakati.

Ujumbe huo ambao unajulikana kama jukwaa la haki jinai unamshirikisha Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) Biswalo Mganga, Naibu Mkurugenzi Upelelezi Makosa ya Jinai nchini (DDCI) Charles Kenyela, Ofisi ya Msajili wa Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Magereza na Jeshi Polisi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...