THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA ZA KISHERIA WALE WOTE WANAOANZA KUJENGA MIJINI KWENYE MAENEO YASIYOPIMWA NA BILA VIBALI VYA UJENZI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen wakati walipoenda kutatua mgogoro wa ardhi wa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa ekari 12,750, ambapo ameagiza eneo hilo lirejeshwe serikalini.

Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi
Serikali kuanzia sasa imewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji kuvunja majengo yote yanayoanza kujengwa katika miji yao bila ya kibali na yale yanayojengwa kwa dhuruma na watu wasio na hati katika viwanja vya watu wengine walio na hati miliki zao za ardhi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameyasema hayo alipofanya ziara wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa alipoenda kutatua mgogoro wa ardhi ambapo ameagiza eneo ya lililokuwa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa ekari 12,750, lirejeshwe serikalini kwa vile utaratibu wa kuligawa umekiukwa kwa kiwango kikubwa, na masharti ya uendeshaji hayajazingatiwa kabisa.

Waziri Lukuvi amesema tatizo la ujenzi holela lianaanza pale ambapo Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wanawaacha majengo yanaibuka katika miji yao bila kujua ujenzi huo una kibali au unajengwa katika kiwanja chenye hati na muhusika wa hati hiyo ndio anayejenga.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji na kuwaagiza kuweka alama za x na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine walio na hati za kumiliki ardhi kwa dhuruma.

“japokuwa serikali inaendelea na kurasimisha maeneo, Hatuwezi kuendelea na zoezi la kufanya urasimishaji wa makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo kinajulikana, kwa hiyo naagiza kuanzia sasa Wakurugenzi, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji kuondoa majengo yote yanayoanza kujengwa bila vibali na ujenzi unaofanywa na watu wanaodhulumu viwanja vya watu masikini” amesema Lukuvi.

 *Lukuvi amesema atapambana na viongozi ambao wataruhusu watu wasio na hati za kumiliki ardhi kujenga katika viwanja vya wamiliki wengine wenye hati zao.*

Waziri Lukuvi amezitaka Halmashauri zote nchini kutoa vibali vya ujenzi katika muda mfupi na kutenga viwanja vingi vilivyopimwa ili kuwapa fulsa wananchi kujenga katika maeneo yaliyopimwa na yaliyopangwa vizuri katika miji yao.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemhakikishia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuwa atayafanyia kazi mapendekezo yake kikamilifu na kwa haraka ili kuondoa migogoro na kero zinazoukabili mkoa wake katika masuala yote ya ardhi.
Baadhi ya viongozi, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wa mkoani Rukwa wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi.

Aidha, katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema Serikali imekusudia kuwanyang’anya mashamba watu wote waliokopeshwa kwa kuyatumia kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye mabenki ndani na nje ya nchi lakini mikopo hiyo hawaitumii kuinufaisha nchi wala kuiendeleza ardhi waliyoitumia kama dhamana.

Waziri Lukuvi ameongeza kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya wawekezaji wengi wenye mashamba makubwa kutumia ardhi kama dhamana kwa ajili ya kupata mikopo kutoka kwenye mabenki ndani na nje ya nchi lakini mikopo hiyo wanaitumia kuwekeza nje ya nchi na kujenga majengo nchi za Ulaya, dubai na kwingine duniani.

Lukuvi amesema Haiwezekani mtu atumie ardhi yetu kujipatia fedha halafu fedha hizo azitumie kuendeleza nchi nyingine na kuiacha ardhi yetu kama pori jambo ambalo linaleta migogoro mikubwa katika jamii inayoyazunguka maeneo hayo.
Baadhi ya viongozi, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wa mkoani Rukwa wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi.

“Kwa hiyo Wizara yangu imekusudia mwezi ujao kupeleka Bungeni marekebisho ya sheria namba 4 ya mwaka 1999 ili kuongeza vifungu ambavyo vitadhibiti mikopo inayopatikana kwa kutumia ardhi kama dhamana” amesema Waziri Lukuvi.

Marekebisho haya tunalenga kuwezesha fedha zinazopatikana kutokana na mikopo iliyotolewa itumike kuendeleza sehemu ya ardhi husika iliyotumika kama dhamana ya kuomba mkopo katika mabenki. Kwa kuwa Tathmini iliyopo inaonesha, baada ya wekezaji hao kupata mikopo kwa kutumia ardhi kama dhamana fedha hizo hawazitumii kuendeleza ardhi husika au katika uwekezaji wowote hapa nchini.

Lukuvi amesema, kuanzia mwezi Novemba tatizo hilo litakwisha kabisa kwa kuwa jukumu hili yatapewa mabenki na wakopeshaji wote ambao watafuatilia kwa karibu maombi ya mikopo kutokana na mpango mkakati uliowasilishwa katika Benki husika.

“na kama Benki husika haitowafuatilia na kuamua kumuachia mtu huyo kwa kuwekeza fedha hizo anavyotaka bila kuendeleza ardhi husika, basi Serikali itamyang’anya mkopeshwaji huyo shamba hilo kwa kuwa atakua amekiuka sheria halafu Benki ambayo itamuachia mtu achukue fedha na asiendeleza shamba lile itakuwa imekula hasara yenyewe” amesema Waziri Lukuvi.