THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

BIASHARA YA CHUMA CHAKAVU NA TAKA HATARISHI KUUZWA NA WALE WENYE VIBALI TU

Tarehe 20 Mei, 2017 Ofisi ya Makamu wa Rais iliutaarifu umma kuhusu utaratibu wa kufanya shughuli zote zinazohusu ukusanyaji, usafirishaji, biashara na urejeleshaji wa taka hatarishi kama vile vyuma chakavu, "Oil" chafu, matairi yaliyotumika, taka za kieletroniki na za umeme na taka zitokanazo na kemikali. 

Ofisi iliwataka wale wote wanaofanya shughuli hizi hapa nchini kufuata sheria, kanuni na miongozo. Aidha, kuzingatia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya mazingira ambayo Tanzania ni mwanachama ikiwa ni pamoja na kuwa na vibali vya biashara husika.

Ofisi inapenda kuukumbusha umma kuwa bado baadhi ya wanaokusanya, kusafirisha na kurejeleza taka hatarishi hawana vibali kama inavyohitajika. Kanuni za Taka Hatarishi za mwaka 2009, kanuni ya 39 hadi 46 zinatoa muongozo wa hatua ambazo zinatakiwa kufuatwa ili shughuli husika zifanyike.

Hivyo, Ofisi inawakumbusha tena wale wote wanaofanya shughuli za uuzaji na ununuzi wa taka hizi kuhakikisha wanafanya biashara na wale wenye vibali tu. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni za Taka Hatarishi za mwaka 2009. 

Aidha, Kanuni ya 47 (3) ya Kanuni za Taka Hatarishi za mwaka 2009 inatoa adhabu kwa mtu ambaye anashindwa kufuata maelekezo yaliyotolewa, ambapo baada ya kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia anaweza kutozwa faini isiyopungua shilingi laki tano (500,000.00) au kifungo kisichopungua mwaka mmoja jela au vyote kwa pamoja. 

Mhandisi Joseph Kizito Malongo

KATIBU MKUU
OFISI YA MAKAMU WA RAIS