ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM), Sadifa Juma Khamis amepandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Mkoa wa Dodoma kwa makosa mawili yanayohusu rushwa.

Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge alifikishwa Mahakamani hapo majira ya 4:55 asubuhi na maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru)akiwa katika gari lenye namba za usajili T994 BEM.

Akisoma kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo Joseph Fovo, Wakili wa serikali kutoka Takukuru Biswaro Biswaro alisema katika kesi hiyo ya jinai namba 232 ya mwaka 2017, mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Desemba 9, mwaka huu akiwa nyumbani kwake maeneo ya Kata ya Mnadani Manispaa ya Dodoma.

Alisema katika kosa la kwanza Sadifa anadaiwa kuwa akiwa nyumbani kwake alitoa rushwa ya vinywaji kwa wajumbe ili wamchague mgombea wa nafasi ya Makamu mwenyekiti wa UVCCM Rashid Mohamed Rashid.

Biswaro alisema kosa la pili analokabiliwa nalo Sadifa ni kutoa ahadi ya kuwalipia gharama za usafiri wajumbe hao kutoka Dodoma –Kagera kama zawadi kwao baada ya kumpigia kura mgombea huyo.

Wakili huyo aliwataja wajumbe hao kuwa ni Kadogo Shabani, Abdallah Hamimu, Octavian Andrea, Didas Zimbihile, Tasinta Nyamwiza, John Lufunga, Mtwawafu Kantangayo, Haleluya Ivody, Deocres Kagunila, Emmanuel Shitobelo, Happiness Rynyogote, Adolf Andrew, Adinani Musheruzi, Editha Domisian na Hashim Abdallah.

Biswaro alisema mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha 15(1)(b) na (2).

Hata hivyo alisema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na upande wa jamhuri unaweka pingamizi la dhamana kwa mshtakiwa.Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Fovo alimhoji mshtakiwa huyo ambapo alikana kutenda makosa yote mawili.


Sababu za kuzuiliwa dhamana 

Wakili Biswaro alisema sababu za kuzuia dhamana ya mshtakiwa huyo kutokana na Mkutano Mkuu wa Uchaguzi UVCCM ni wa siku mbili mfululizo 10-11 Desemba 2017 na matokeo bado hayajatangazwa hivyo kuna uwezekano wa kuingilia uchaguzi huo.

“Naomba Mahakama itambue uchaguzi bado unaendelea na mshitakiwa hadi sasa hajakabidhi uongozi bado ni mwenyekiti,”alisema

Aidha alisema sababu nyingine ni kuwa mashahidi wengi ni viongozi ambao ni Mwenyekiti na Makatibu na endapo akiachiwa kwa dhamana ana kila aina ya ushawishi anaweza kuvuruga upelelezi.

Kufuatia maelezo hayo, Wakili wa utetezi Godfrey Wasonga alipinga kuzuiwa kwa dhamana na kudai kuwa ni haki ya mtu kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Alibainisha kiapo cha kuzuia dhamana hicho kilichowasilishwa mahakamani ambacho kimetolewa na Emma Kuhanga (Kamanda wa Takukuru Dodoma) hakina mashiko.

“Uchaguzi wa UVCCM umeshaisha na mshindi tayari ameshapatikana na hakuna uchaguzi mwingine wa kuingilia au kama kuna uchaguzi utafanyika kiapo kingesema,”alisema Wasonga

Alihoji sababu za kupelekwa kesi ambayo haijakamilika upelelezi na kuzuia dhamana kwa mshtakiwa na kwamba mshtakiwa huyo hataweza kuingilia uchunguzi kwa sababu walizozitoa.“Hawa mashahidi atawezaje kuwashawishi wakati mtu ameshatoka madarakani?mteja wangu ni mbunge ni mtu makini na anaaminiwa asihukumiwe kwa kuwekwa ndani kwasababu zisizo na mashiko,”alisema Wasonga.

Aliomba Mahakama itupilie mbali pingamizi hilo na mshtakiwa apewe dhamana kwa kuwa hataweza kuingilia uchaguzi na uchaguzi mwingine wa Umoja huo ni hadi mwaka 2022.

Kutokana na mvutano huo, Hakimu Fovo aliahirisha kesi hiyo hadi desemba 19, mwaka huu na kwamba Mahakama ndipo itatoa maamuzi kuhusu suala hilo na mshtakiwa ataendelea kuwa rumande.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...