THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Kaimu Mkurugenzi TAA, Ataka Madereva Wa Magari Ya Zimamoto kuyatunza

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela amewataka madereva wanaoendesha magari ya zimamoto na uokoaji kwenye viwanja vyote vya ndege Tanzania kuyathamini na kuyatunza magari hayo kwa kuwa wameaminiwa kufanya kazi hiyo.

Bw. Mayongela alitoa kauli hiyo kwenye Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), alipokwenda kujitambulisha na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili, ambapo alisema magari hayo yamenunuliwa kwa gharama kubwa, hivyo yanapaswa kutunzwa.

Alisema uthamini wao kwa magari hayo kutayafanya kudumu na kuyafanya kazi kwa muda mrefu bila kuharibika, jambo ambalo litachangia ufanisi wa kazi, ya uokoaji na usalama kwenye viwanja vya ndege, ambapo mbali na miundombinu pia lazima miundombinu ipewe kipaumbele.

“Najua wapo wenzenu wachache sio waaminifu wamekuwa wakitengeneza manunuzi hewa ya vifaa na hata mafuta kwa manufaa yao binafsi, lakini ninawaomba mujione nyie ndio wenye thamani kwa kuaminiwa kuendesha magari haya ya mamilioni ya fedha, kwani ni nyie tu mnayoweza kuyaendesha kutokana na kuwa na mitambo ya kisasa tofauti kidogo na mengine, hivyo basi tuyatunze ili tuisaidie serikali yetu isiingie gharama za mara kwa mara za kununua vifaa au magari mengine mapya,” alisisitiza Bw. Mayongela.

Hatahivyo, alisema zimamoto ni moja ya mambo ya msingi hivyo amewahakikishia kuwapeleka kozi za mara kwa mara za ndani na nje ya nchi, kutokana na mambo mbalimbali yanayobadilika duniani, na kwa kuanzia ataanza na askari wawili hadi wanne, kulingana na mafunzo wanayostahili kushiriki, na atahakikisha washiriki ndio wanaokwenda kufanyia kazi kwa vitendo katika utendaji wao na sio kupeleka mabosi ambao hawahusiki.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama mbele), akiongea na askari wa zimamoto na uokoaji wa kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). Mbele kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Johannes Munanka na (kulia) ni Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege nchini, Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa.

Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka (aliyesimama mbele) akitoa maelezo mbalimbali kwa askari wa zimamoto na uokoaji katika kikao kilichoitishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela.
Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa (aliyesimama) akiongea na askari wa kituo cha zimamoto na uokoaji cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, katika mkutano ulioitishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela.