Na Ramadhani Juma, 
HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imeanza utekelezaji wa agizo la Serikali la kila Halmashauri nchini kuhakikisha inaangamiza vimelea vya mbu waenezao ugonjwa wa Malaria kwa kupulizia dawa katika maeneo yote ambayo ni rafiki kwa vimelea hivyo kukua.
Utekelezaji wa agizo hilo umeanza jana Jumanne Desemba 12, 2017 na litadumu kwa siku saba, ambapo watakaohusika na upuliziaji ni watumishi sita (6) kutoka Ngazi ya Halmashauri na Wanajamii sitini (60) wa kujitolea kutoka katika Kata 41 za Manispaa ya Dodoma.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Hamad Nyembea amesema maeneo ambayo yatapuliziwa dawa kwa ajili ya kushambulia vimelea hivyo ni pamoja na maeneo ya Mabwawa yakiwemo mabwawa ya Maji Taka, madimbwi yanayotuamisha maji, makorongo, mifereji, na matenki yanayotumika kuhifadhia maji majumbani.
Zoezi hili ni shirikishi ambapo ngazi zote za uongozi katika Wilaya zitashiriki kwa namna moja au nyingine katika usimamizi, kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Madiwani, Menejimenti ya Halmashauri, Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Afya ya Halmashauri, Viongozi wa Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
Kwa Mujibu wa Daktari Nyembea, dawa inayopuliziwa ni mahususi kwa ajili ya kushambulia vimelea vya mazalia ya Mbu tu, na haina madhara yeyote kwa binadamu hivyo amewataka wakazi wa Manispaa kutokuwa na hofu yeyote kwani zoezi  hili ni muendelezo wa vita ya muda mrefu ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria nchini.
Alitoa wito kwa Wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiano utakaohitajika wakati wa zoezi la upuliziaji, ambapo wadau mbalimbali pia watashirikishwa ikiwemo Vyombo Vya Habari, Viongozi wa Dini, Watu maarufu, na Taasisi mbalimbali.
Kikosi kazi kinachofanya zoezi la kupulizia dawa ya kuua vimelea vya mazalia ya Mbu waenezao ugonjwa wa Malaria katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kikiendelea na kazi hiyo katika maeneo mbalimbali baada ya kuanza kwa zoezi hilo hilo jana. Picha kwa hisani ya Ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Dodoma

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...