WILAYA YA MUHEZA, TANGA, TANZANIA – Katika sherehe zilizofanyika katika kijiji
kimoja huko mkoani Tanga, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani
(WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) yaligawa
tableti zilizowekewa mfumo wa elimu kwa watoto. Tableti hizo ziligawiwa kama sehemu ya
mradi wa majaribio wa miezi 15 chini ya Global Learning XPRIZE, ambao ni mradi wa miaka
mitano uliotokana na mashindano duniani yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 15.
Mradi huu wa dunia unatoa changamoto kwa timu za wabunifu kubuni na kuandaa zana-
wazi za kiteknolojia ili kuwawezesha watoto walio na fursa ndogo ya kupata elimu katika
umri wa miaka tisa hadi kumi na mmoja, kujifunza wenyewe stadi za msingi za Kusoma,
Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Kama sehemu ya majaribio, zaidi ya watoto 2,400 kutoka katika vijiji 167 katika wilaya za
Handeni, Korogwe, Lushoto, Mkinga, Muheza, na Pangani watapewa tableti mpya ya aina ya
Google Pixel C, zilizotolewa kwa hisani ya Google. Tableti hizo zimewekewa mifumo ya elimu
kutoka kwa washindi watano wa mwisho wa Global Learning XPRIZE. Washindi hawa
walichaguliwa kutoka katika timu 198 na paneli ya majaji 11 wa kujitegemea na walio
wataalamu na kutangazwa mwezi September, 2017 wakati wa wiki ya Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa.
“Teknolojia hii inayowawezesha watoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu pasipo
msaada wa mwalimu, ni ubunifu wa kiwango cha juu kabisa,” alisema Mayasa Hashim
ambaye ni Afisa Elimu Mkoa wa Tanga. “Msaada huu utaleta matokeo mazuri katika
kuwakomboa watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ili kwamba na wao wajifunze stadi
hizi.”
Tableti hizo ziligawiwa na WFP kwa sababu shirika hili linasimamia uendeshaji wa kitengo
cha lojistiki na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) cha majaribio katika mazingira
halisi. Jukumu lake ni pamoja na kuingiza zana hiyo ya kiteknolojia katika tableti, kuanzisha
vituo vya kuwekea umeme unaotokana na jua kwenye tableti hizo vijijini na kusimamia
matengenezo, marekebisho na kutoa tableti mpya katika kipindi chote cha majaribio ya
ugani.
SOMA ZAIDI HAPA
SOMA ZAIDI HAPA
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...