THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

AZAM YAMINYWA NA MAJIMAJI, YAKUBALI SARE YA 1-1

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Majimaji katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika leo mchana kwenye Uwanja wa Majimaji, mjini Songea mkoani Ruvuma.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kufikisha pointi 27 na kuwa katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi baada ya   Simba kupata ushindi dhidi ya Singida na kukaa  kileleni kwa pointi 29.

Azam FC ndiyo iliyoanza kuliona lango la Majimaji dakika ya 30 kupitia bao safi la winga Joseph Mahundi, aliyeunganisha kiustadi pasi safi ya mshambuliaji Yahya Zayd, bao lililodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.

Kipindi cha pili Azam FC iliwaingiza nyota kadhaa kwenye dakika tofauti wakiingia viungo Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji Shaaban Idd, ikiwatoa Bernard Arthur, Salmin Hoza na Idd Kipagwile, mabadiliko ambayo yaliongeza kasi ya mashambulizi wakati timu hiyo ilipokuwa ikishambulia.

Dakika ya 73 Majimaji iliweza kusawazisha bao hilo kupitia kwa Marcel Boniventure, aliyepiga mpira wa moja kwa moja wa kona uliojaa wavuni na kufanya matokeo kuisha kwa sare hiyo.

Kama Azam FC ingekuwa makini ingeweza kujipatia mabao mengine kupitia nafasi walizopoteza kwenye mchezo huo, kipindi cha kwanza kupitia kwa Bernard Arthur, kipindi cha pili ikipoteza nyingine kwa washambuliaji wake Yahya Zayd, Shaaban Idd na beki Yakubu Mohammed.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuelekea mkoani Mbeya kesho Ijumaa asubuhi tayari kabisa kwenda kucheza na Tanzania Prisons, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Sokoine Jumapili hii.