THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

HII NDIO ASILI YA JINA LA MKOA WA MBEYA

 Mkoa wa Mbeya ni moja kati ya Mikoa 32 ya Tanzania, unapatikana nyanda za juu kusini mwa nchi yetu hii. jina la mkoa wa Mbeya ni neno la kiasili la kabila la Kisafwa lilikuwa likitamkwa ‘Ibheya’ likiwa na maana chumvi. Inaelezwa kuwa wafanyabiashara wengi walikuwa wakifika eneo hilo kwa biashara ya kubadilishana chumvi na mazao yao.

Inaelezwa kuwa mji wa sasa wa Mbeya ulianzishwa na wakoloni Waingereza mnamo mwaka 1927 kufuatia kushamiri kwa upatikanaji wa dhahabu kwenye milima ya Loleza na mkondo wake uliokwenda mpaka kufika mji wa Chunya.

Wakazi wenyeji wa mkoa wa Mbeya ni wa kabila la Wasafwa ambao wamekuwa wakihamia milimani kupisha wageni. Kukua kwa kasi kwa jiji la Mbeya kumepelekea wenyeji hao kuuza maeneo yao na wao kurudi maeneo ya milimani wakiendelea kujishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji kidogo. 
 Mkoa wa Mbeya kwa sasa una wilaya nne, hii ni baada ya kugawanywa kwa mkoa huo na Mkoa wa Songwe ambao nao pia umebakiwa na wilaya nne ambazo ni Ileje, Chunya, Mbozi na Momba. 

Leo hii eneo la wilaya ya Mbeya ambako ndipo jiji lilipo limetawaliwa zaidi na Wanyakyusa na Wakinga wakiwa ndiyo wafanyabiashara wakubwa na Wahindi pia.

Wenyeji wengine wa Mbeya ni watu wa kabila la Wamalila, Wenyeji wa wilaya za Rungwe na Kyela ni Wanyakyusa Wenyeji wa wilaya ya Mbarali ni Wasangu, Wawanji, Wabena na Wakinga.

Wenyeji wa wilaya ya Ileje ni Wandali, Wenyeji wa wilaya ya Chunya ni Wabungu ingawa watu waishio huko zaidi ni Wanyiha. Wenyeji wa wilaya ya Mbozi ni Wanyiha na Wanyamwanga, lakini mji wa Tunduma umetawaliwa zaidi na Wakinga ambao ndiyo wafanyabiashara wenye kumiliki uchumi wa mji huo mdogo.