Na Lilian Lundo na Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA
Watanzania washauriwa kusajili na kutumia kikoa cha dot tz (.tz) na dot Africa (.africa) katika matumizi ya intanenti kwa ajili ya kutoa utambulisho wa kitaifa, ki-bara na kukuza uchumi wa Taifa na Bara la Afrika.

 Akizungumza leo Mjini Dodoma Mkurugenzi Mtendaji wa Registry.Afrika Lucky Masilela amesema kuwa vikoa hivyo vinafaida mbalimbali ikiwemo kupunguza gharama za mawasiliano na pia kukuza uchumi wa nchi na bara zima la Afrika kutokana na fedha zinazotumika kusajili vikoa hivyo hubaki katika nchi na bara husika.

“Nitoe ombi kwa wale wote wanaotumia mtandao watumie mtandao wa dot tz au dot Afrika kwa sababu vikoa vingine haviwezi kusaidia Afrika, kutokana na fedha zinazotumika kusajili vikoa hivyo hubaki katika nchi husika” ameongeza Masilela.

Aidha, Masilela amefafanua kuwa Umoja wa Afrika (AU) uliridhia maombi ya rajisi ya dot africa kufanya kampeni ya matumizi ya kikoa cha dot Africa, ambapo Rajisi ya dot africa iliainisha maeneo matano (5) ya kufanya kampeni hiyo kwa niaba ya bara lote la Afrika. Maeneo hayo ni Afrika ya Mashariki, Afrika ya Kaskazini, Afrika ya kati, Afrika Magharibi na Afrika ya kusini.

“Lengo kuu la kampeni hii ni kuwahamasisha waafrika wote watumie kikoa cha dot africa na pia kujenga hamasa ya waafrika kujivunia uafrika wao na kujenga uchumi unaotegemea rasilimali ya kikoa hiki pekee kinacho watambulisha na kuwaunganisha waafrika wote” ameongeza Masilela.

Vile vile amesema kuwa kampeni hiyo inaudhihirishia ulimwengu kuwa ucheleweshwaji wa rasilimali pekee ya kuwatambulisha waafrika wote  kwenye mtandao wa Intaneti umefikia hatima yake hivyo Waafrika sasa, kwa kutumia kikoa cha dot africa  wanauwezo wa  kuwasiliana, kutoa huduma, kufanya biashara (taasisi za umma na binafsi) bila bugudha yoyote katika mtandao wa Intaneti.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Network Information Centre Mhandisi Abibu Ntahigiye amesema kuwa rajisi ya dot africa (ZACR) ilipewa mamlaka ya kuendesha rajisi ya dot africa mwezi Februari 2017 ikiwa ni baada ya miaka mitano (5) ya juhudi za kutafuta uhalali wa kufanya hivyo.

“Kufuatia mafanikio hayo, timu ya dot africa ilipewa jukumu na Umoja wa Africa (Africa Union - AU) kuendesha kampeni za kuhamasisha matumizi ya kikoa cha dot africa barani kote kwa kipindi cha miezi sita (6) kuanzia Agosti 2017 mpaka Januari 2018” ameongeza.

Naye Mwanasheria wa Rajisi ya Tanzania (.tz) Sarah Mhamilawa amesema matumizi ya dot tz ni rahisi na panapotokea tatizo la kiufundi muhusika anapiga simu .tz na tatizo hutatuliwa papohapo tofauti na vikoa vingine ambavyo huhitaji kufuata mlolongo uliowekwa kwa ajili ya utatuzi wa tatizo husika ambao huchukua muda kutatuliwa.

Kampeni ya matumizi ya  dot africa imeambatana na kuendesha magari (roadshow) wakiwa na Bendera ya  dot africa kutoka Afrika Kusini ambapo safari ilianza Januari 1, 2017 kuelekea Addis ababa, Ethiopia kupitia Botswana, Zimbabwe, Zambia, Tanzania na Kenya.

Aidha timu hiyo ikiwa Tanzania imeanzia kampeni hiyo Tunduma kupitia Iringa, Dodoma, Arusha na Kilimanjaro ambapo wakiwa Kilimanjaro watapandisha bendera ya dot Africa na dot tz kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro.


  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzania Network Information Centre Mhandisi Abibu R. Ntahigiye (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kampeni ya msafara kwa njia ya barabara (Roadshow Campaign) inayofanywa na taasisi ya Dot tz na Dot africa kuhamasisha matumizi ya mitandao hiyo ya intaneti kwa Afrika leo mkoani Dodoma. Kulia kwake ni  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Registry.Africa Ndg. Lucky Masilela.
  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Registry.Africa Ndg. Lucky Masilela(wakwanza kushoto) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kampeni ya msafara kwa njia ya barabara (Roadshow Campaign) inayofanywa na taasisi ya Dot tz na Dot africa kuhamasisha matumizi ya mitandao hiyo ya intaneti kwa Afrika leo mkoani Dodoma. Katikati ni  Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzania Network Information Centre Mhandisi Abibu R. Ntahigiye na mmoja wa wajumbe wa msafara huo Ndg. Ronald Schwaerzler
 Mmoja wa wajumbe wa msafara kwa njia ya barabara (Roadshow Campaign) inayofanywa na taasisi za mitandao ya intaneti za Dot tz na Dot africa kuhamasisha matumizi ya mitandao kwa Afrika Ndg. Ronald Schwaerzler (wapili kulia) akifafanua kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu ratiba ya kupanda mlima Kilimanjaro kama sehemu ya kampeni hiyo leo mkoani Dodoma. Wakwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Registry.Africa Ndg. Lucky Masilela na wapili ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Tanzania Network Information Centre Mhandisi Abibu R. Ntahigiye
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dododma Ndg. Jabera Matogolo(wakwanza kulia) akielezea namna ambavyo mtandao wa intaneti unavyosaidia kukuza kiswahili wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu kampeni ya msafara kwa njia ya barabara (Roadshow Campaign) inayofanywa na taasisi ya Dot tz na Dot africa kuhamasisha matumizi ya mitandao hiyo ya intaneti kwa Afrika leo mkoani Dodoma.
Washiriki wa kampeni ya msafara kwa njia ya barabara (Roadshow Campaign) inayofanywa na taasisi ya Dot tz na Dot africa kuhamasisha matumizi ya mitandao hiyo ya intaneti kwa Afrika wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma walipokutana na waandishi wa habari leo mkoani Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...