*Asema suala la ndoa kwa sasa kwake bado analitafakari...

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

UNAPOAMUA kuzungumzia au kutaja majina ya wasanii wa kike ambao wanajihusisha na muziki wa kizazi kipya a.k.a Bongo Fleva basi lazima utakutana na jina la Nuru The Light. Jina halisi la mwadada huyo ni Nuru Magram lakini kwenye muziki basi kama ambavyo wanafanya wasanii wengi tu wa ndani na nje ya Tanzania akaamua kuwa na a.k.a yake.

Nuru The Right ni moja kati ya wasanii ambao wanaheshima kutokana na kazi zao za muziki wa kizazi kipya.Moja ya wimbo alioutoa kwa mashabiki wake na kumfanya atambulike na kuwa maarufu zaidi ni wimbo wake wa Walimwengu, licha ya kwamba ni juzi tu ameipua wimbo mpya unaojulikana kwa jina la Nimeachwa.

Mbali ya muziki amekuwa akifanya mambo mengine mbalimbali na kwa sehemu kubwa anaishi nchini Swedeen, lakini kwa sasa amerejea nchini kusalimia ndugu, jamaa na marafiki.

Sifa kubwa ya Nuru The Right ni msanii wa kike ambaye anafahamu nini ambacho anakifanya katika muziki. Anajua wakati gani wa kutoa wimbo mpya na wakati gani wa kusoma soko la muziki linakwendaje.

Globu ya Jamii imepata nafasi ya kutembelewa na msanii huyo ambaye hana makuu, hana sifa za kijinga na siku zote amekuwa mnyenyekevu, mpole , mcheshi na mwenye kuheshimu kila mtu na kubwa zaidi ni msanii ambaye sauti yake inaweza kumtoa nyoka pangoni. Hakika ni msanii anayejali mashabiki wake.

Akiwa katika ofisi za Michuzi ameulizwa maswali mengi na kwa sehemu kubwa ameyajibu kadri ya uwezo wake.Hata hivyo moja ya swali ambalo ameulizwa lilikuwa linataka kufahamu kama ameolewa au la, Nuru The Light akatabasamu na kutoa sauti ya kicheko na kujibu kuwa kwa sasa hana mume, kwani wakati wa kuolewa na kuwa mke wa mtu bado hajafikiria kwa sasa.

Licha ya kwamba bado hajaolewa lakini anasema wakati ukifika kama mwanamke atahitaji kuwa na mume lakini si tu ilimradi mume, bali awe anasifa ambazo anahitaji kutoka kwa huyo ambaye atataka kumuoa.Kwanini hajafikiria kuolewa amejibu kuwa wakati haujafika bado kwani haipo kwenye mipango yake kwa sasa.
Nuru The Right hakusita kuelezea baadhi ya sifa ambazo anataka kuwa nazo mtu ambaye atataka kumuoa.Moja ya sifa ambazo anataka awe nazo mwanaume atakayetaka kumuoa ni mwanaume ambaye anajitambua, anajali na kubwa zaidi awe mwenye imani ya dini na kumjua Mungu.

"Zipo sifa nyingi za aina ya mume ambaye nataka awe nazo , lazima niwe na mwanaume ambaye anajitambua na anaelewa anachokifanya.Pia awe mwanaume mwenye imani ya dini,"amesema Nuru The Right huku akionesha kuwa zipo sifa nyingine nyingi ambazo anatamani mume atakeyemuoa awe nazo.

Alipoulizwa kama anazungumzia vipi aina ya maisha ya baadhi ya wasanii ambayo yanaonesha kutotulia kwenye mahusiano yao ya kimapenzi, amejibu kuwa binafsi hafurahishwi na tabia hiyo kwani anapofanya msanii mmoja inaonekana ndio tabia ya wasanii wote wakati si kweli.

"Binafsi najiheshimu na wakati mwingine ninaposikia habari za wasanii na mambo ambayo wanayafanya huwa inaniumiza sana moyo.Ni vema wasanii tukawa makini na aina ya staili ya maisha yetu.

"Hata hivyo kuna mambo ambayo wakati mwingine yanakera.Unaweza kukuta msanii fulani anafanya mambo ambayo yanavunja heshima yake lakini hakuna ambaye anamsema wala kumwambia

"Ila akitokea msanii mwingine akafanya hivyo hivyo watu wanakuja juu na kuanza kutoa maneno ya kila aina.Ni kama vile kuna wasanii wakifanya sawa na wengine wakifanya wanakosea,"amesema Nuru The Right.

Baada ya kukuleza sehemu ndogo tu kati ya mengi ambayo msanii huyo ameyazungumza kuhusu maisha yake ya muziki na nini ambacho amepanga kukifanya, usikose kufuatilia hatua moja baada ya nyingine ya maswali na majibu ya msanii huyo kwa kuangalia hiyo video hapo chini. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...